NEWS

Thursday, 23 March 2023

Serikali wilayani Tarime yakifunga chuo cha St Collins



Na Mwandishi Wetu, Tarime
-------------------------------------------

SERIKALI wilayani Tarime, Mara imekifunga kwa muda chuo binafsi cha St Collins kilichopo eneo la Rebu mjini Tarime, baada ya kubaini uwepo wa mazingira hatarishi kwa wanafunzi na ukosefu wa walimu, miongoni mwa matatizo mengine.

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo iliyofuatana na wataalamu wa elimu, imefikia uamuzi wa kuagiza chuo hicho kifungwe baada ya kukitembelea na kukikagua leo Machi 23, 2023.

“Tumepita kukagua miundombinu ya chuo chenu baada ya kupitia taarifa mbalimbali kutoka ofisini. Kuna mapungufu mengi ambayo tumeyaona. Mfano malazi hayakidhi vigezo vya kuwa malazi kwa wanachuo,” Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele amesema wakati akitangaza maamuzi hayo mbele ya wananchuo wa chuo hicho.

Kanali Mntenjele amesema pia imebanika kuwa chuo hicho hakina jiko – hali ambayo amesema kiusalama haikubaliki.

Ukaguzi huo umebaini uwepo wa mazingira yasiyo rafiki katika bweni la wavulana, ambapo baadhi ya wanafunzi wa kike wakiwemo wagonjwa wamekutwa wakiwa ndani yaje, jambo ambalo pia Kanali Mntenjele amesema halikubaliki.

Mapungufu mengine yaliyobainika ni pamoja na chuo hicho kutokuwa bafu - hali ambayo inawazimu wanafunzi kutumia maeneo yasiyo rasmi kuoga.

Imebainika chuo hicho pia hakina walimu wa kutosha na wachache waliopo hawan sifa na mikataba ya kazi.

Hivyo mmiliki wa chuo hicho ametakiwa kufanya marekebisho ya mapungufu hayo ili kukidhi mahitaji yanayotakiwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa.

Kanali Mntenjele (katikati) akitangaza kukifunga chuo hicho

“Tunakifunga kwa muda wa miezi mitatu mmiliki afanye marekebisho, tutatuma wataalamu wetu wakague, tukijiridhisha chuo kitafunguliwa na siyo vinginevyo,” amesisitiza Kanali Mntenjele.

Chuo hicho ambacho kinatoa kozi mbalimbali kinaripotiwa kuwa na wanafunzi wa kike na kiume ambao idadi yao haikufahamika mara moja, huku kikiwa na walimu watatu.

Mkuu huyo wa wilaya amesema mwenendo wa chuo hicho haukubaliki na kuwataka wanafunzi wa chuo hicho kuwambia wazazi wao ukweli wa hali halisi ya mazingira iliyopo chuo hapo.

“Muwambie wazazi wenu chuo hiki hakina sifa. Manasoma nini, chuo hakina walimu? amehoji Kanali Mntenjele.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages