NEWS

Monday 12 August 2024

Mashindano ya Mahusiano Cup 2024 yazinduliwa kwa kishindo Nyamongo



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Maulid Surumbu (mwenye kofia nyeupe), Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko (katikati mwenye fulana ya bluu) na viongozi wengine wakiingia uwanjani kukagua timu wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Mahusiano Cup 2024 jana.
---------------------------------------------------

NA MWANDISHI WETU, Tarime
------------------------------------------

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Maulid Surumbu ameongoza uzinduzi wa mashindano ya soka ya Kombe la Mahusiano - maarufu kwa jina la Mahusiano Cup yanayodhaminiwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Uzinduzi huo ulifanyika jana kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Ingwe iliyopo Nyamongo, kata ya Kemambo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara.


Timu zilizopata nafasi ya kuchuana katika uzinduzi wa mashindano hayo mwaka huu, ni Kewanja FC na Nyamwaga FC ambazo zilitoka droo ya bila kufungana.

Mashindano hayo yataanza kutimua vumbi rasmi Agost 14, mwaka huu ambapo timu 15 zitashiriki, ikiwemo ya wafanyakazi wa mgodi wa North Mara.

Lengo la mashindano hayo ambayo huandaliwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kila mwaka, ni kudumisha na kuendeleza mahusino kati ya mgodi huo na jamii.

Kaulimbiu ya mashindano hayo inasena “Mahusiano Bora kwa Uwekezaji Endelevu.”

“Hii ni michuano ya kirafiki inayolenga kudumisha mahusiano kati ya jamii na mgodi, na michezo ni afya, inatuepushia magonjwa yasiyo ya kuambukizwa,” alisema DC Surumbu.

Awali, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko alisema michezo ni ajira, afya, inaibua vipaji mbalimbali, na kwamba Mahusiano Cup ni kwa manufaa ya pande zote mbili [jamii na mgodi].

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kemambo, Bogomba Rashid alitumia fursa hiyo kukemea vitendo vya kuvamia na kufanya uhalifu katika mgodi wa North Mara.

"Wanamichezo na mashabiki, tumekuja kudumisha mahusiano bora. Suala la uhalifu [mgodini] tuseme sasa basi, tutumie kile kilicho halali,” alisisitiza Bogomba.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick Gold kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages