
Lori likiwa kazini katika Mgodi
wa Dhahabu wa North Mara.
Madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara yaliyotolewa na baadhi ya wakazi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo wilayani Tarime, yamegonga mwamba baada ya Mahakama ya Juu ya Ontario nchini Canada kuamua kwamba hayana msingi wowote.
Madai hayo ya kukiukwa haki za binadamu yalikuwa yakitolewa na asasi chache zisizokuwa za kiserikali zenye mrengo wa kiharakati zilizodai kwamba Jeshi la Polisi lilikuwa likiwanyasa wananchi katika maeneo yanayozunguka mgodi wa North Mara.
Taarifa iliyotolewa jana na Barrick kutoka jiji la Toronto, Canada ilisema Mahakama ya Ontario haikuwa jukwaa mwafaka la kusikiliza madai hayo, na hivyo kuyatupilia mbali kwa kutokuwa na msingi wowote.
Kampuni ya Barrick inayoendesha migodi ya dhahabu ya North Mara wilayani Tarime, Mara na Bulyanhulu wilayani Kahama, Shinyanga chini ya Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wake, Dkt Mark Bristow, huko nyuma ilikuwa mara kwa mara ikikanusha madai hayo kwamba hayana ukweli wowote.
Uamuzi wa Mahakama hiyo ya Ontario umekuja kama faraja kwa Barrick kutokana na ushirikiano imara na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
“Tunajivunia mafanikio tuliyoyapata nchini Tanzania kutokana na ushirikiano wetu na serikali ya nchi hiyo kupitia ubia wa Twiga,” alisema Dkt Bristow.
“Mchango wa mapato ya migodi yetu umeleta mageuzi katika uchumi wa nchi hiyo. Uwekezaji wetu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wenyeji, ukiambatana na mkakati wetu wa kuleta maendeleo ya jumla, umeboresha hali za maisha,” aliongeza.
Kesi hiyo ya madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu ilifikishwa mbele ya Jaji J. Akbarali.
No comments:
Post a Comment