Mwakilishi wa Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Julia Kronberg na Meneja Miradi wa FZS- Serengeti, Masegeri Rurai wakifurahia jambo wakati wa uzinduzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Manchira.
-----------------------------------------------
HUENDA vikwazo vya elimu kwa wanafunzi wa kike vikabaki historia katika Shule ya Sekondari Manchira iliyopo wilayani Serengeti, baada ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) kuwajengea bweni la kisasa kwa gharama ya shilingi milioni 334.
KfW imrfadhili ujenzi wa mradi huo kupitia Shirika la Frankfurt Zoological (FZS), kwa lengo la kuhamasisha uhifadhi na maendeleo ya ikolojia ya Serengeti.
Bweni hilo lenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 60 kwa wakati mmoja, lilizinduliwa Novemba 12, 2024 na Mwakilishi wa Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Julia Kronberg.
“Mradi huu ni miongoni mwa mingi iliyotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Ujerumani na Tanzania ili kunufaisha jamii zinazoishi jirani na maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori.
“Ninaamini bweni hili litatunzwa vizuri ili liwe endelevu sio tu kwa manufaa ya wanafunzi kutoka kata ya Manchira, bali pia jamii nzima ndani na nje ya wilaya ya Serengeti,” alisema Julia ambaye aliambatana na wataalamu mbalimbali kutoka Serikali ya Ujerumani na KfW.
Aliwashukuru watu wote wanaoshiriki kwa namna mbalimbali katika kuhifadhi ikolojia ya Serengeti akisema ujenzi wa bweni hilo ni sehemu ya matunda ya jitihada hizo.
“Haki ya maendeleo kwa wananchi na lengo la kimataifa la kulinda wanyamapori na viumbe hai vina umuhimu sawa. Lakini ikiwa jamii haziwezi kufaidika usawa unakosekana. Tunaamini kwa dhati kwamba upatikanaji wa huduma za kijamii ni kipengele muhimu cha kuthibitisha usawa,” alisema.
Aidha, Julia alieleza kuridhishwa na utendaji wa TANAPA akisema ni mdau mwaminifu wa Serikali ya Ujerumani katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani na nje ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Viongozi mbalimbali, walimu na wanafunzi wakifurahia picha ya pamoja juzi, wakati wa uzinduzi bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Manchira wilayani Serengeti, lililojengwa na TANAPA na KfW.
----------------------------------------------
Kwa upande wake Afisa Uhifadhi Mkuu (CPO) kutoka TANAPA, Nuhu Daniel Masay alisema ujenzi wa bweni hilo ni alama ya kuendeleza ujirani mwema kati ya hifadhi na jamii.
“Miundombinu ya elimu kama hii ni miongoni mwa miradi ya kijamii tunayoipa kipaumbele ili kuendeleza ujirani mwema. Tunaamini kwamba jamii iliyoelimika itaunga mkono uhifadhi,” alisema CPO Masay.
Alitumia nafasi hiyo pia kuishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kuendelea kuwekeza kwenye masuala ya uhifadhi wa wanyamapori na mazingira kupitia shirika la FZS.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Eric Ngole naye aliishukuru Serikali ya Ujerumani, TANAPA na FZS kwa kutekeleza mradi huo. “Hiki mlichokifanya ni kikubwa sana, endeleeni na moyo huo huo,” alisema.
Walimu, wanafunzi na wazazi mbalimbali walieleza kupokea mtadi huo kwa furaha kubwa wakiamini utakuwa mkombozi wa elimu kwa wanafunzi wa kike katika shule hiyo.
Mkuu wa Shuke ya Sekondari Manchira, Mwalimu Alhaji Shemtandulo alishukuru na kuweka wazi kwamba mradi huo wa bweni utaisaidia shule hiyo kutatua changamoto zilizokuwepo.
“Wanafunzi wanaoenda kunufaika na bweni hili wamekuwa wakitembea umbali mrefu hali inayopunguza ari ya kupenda shule, lakini pia kushusha taaluma. Mradi huu pia utasaidia kupunguza utoro kwa wanafunzi wa kike,” alisema Mwalimu Shemtandulo.
Mwanafuzi wa kidato cha tatu, Penina Richard Nyambache ambaye pia ni Kiranja Mkuu wa shule hiyo naye alisema bweni hilo litakuwa chachu ya maendeleo ya elimu kwa watoto wa kike.
Wakazi wa kijiji cha Rwamchanga ilipo shule hiyo, Samwel Nyakande na Samwel Paul walijivunia mradi huo wakisema utasaidia kupunguza tatizo la mimba kwa wanafunzi kutokana na vishawishi vya kupewa lifti na waendesha pikipiki wakati wa kwenda na kutoka shule.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Majaliwa awatembelea majeruhi Muhimbili
>>Benki Kuu ya Tanzania yawanoa waandishi wa habari Kanda ya Ziwa kuhusu masuala ya fedha, akiba ya dhahabu na uchumi wa nchi
>>PSSSF yalipa trilioni 10.46 kwa wanufaika zaidi ya 300,000 tangu ianzishwe miaka 6 iliyopita
>>Askari Uhifadhi auawa na tembo Tarime Vijijini
No comments:
Post a Comment