NEWS

Tuesday, 10 December 2024

Mgodi wa North Mara wawapa wanawake msaada wa majiko 222 ya gesi



Waziri Dkt Dorothy Gwajima akikabidhi majiko ya gesi kwa baadhi ya wanawake kutoka vijiji vinavyozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara jana Desemba 9, 2024. (Picha zote na Mara Online News)
---------------------------------

Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa kushirikiana na Kampuni ya Taifa Gas umetoa msaada wa majiko 222 ya gesi ambayo yamekabidhiwa kwa baadhi ya wanawake kutoka vijiji 11 vinavyouzunguka.

Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Apolinary Lyambiko, majiko hayo yametolewa kuunga mkono jitihada za serikali za kumtua mama kuni kichwani na kumuepushia adha ya matumizi ya nishati ya kupikia isiyo salama.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt Dorothy Gwajima alikabidhi majiko kwa wanawake wakati wa maadhimisho ya kilele cha kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyofanyika kitaifa Nyamongo, wilayani Tarime jana.

Wakati huo huo, mgodi wa North Mara kwa mara nyingine tena, umevipatia vijiji vitano vilivyo jirani gawio la mrahaba la shilingi bilioni 2.1, ikiwa ni malipo ya robo ya pili ya mwaka 2024.

Vijiji hivyo na kiasi cha malipo kikiwa kwenye mabano ni Genkuru (746,461,112), Nyangoto (581,176,695), Kerende (454,221,570), Nyamwaga (225,997,310) na Kewanja (98,350,773).

Waziri Gwajima aliupongeza mgodi wa North Mara akisema utoaji wa gawio la mirahaba hiyo unasaidia kuboresha huduma za jamii na kuchochea maendeleo ya kisekta katika vijiji hivyo.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages