
Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Faraja Ng'ingo (kulia) akikabidhi msaada wa madawati 200 kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Salum Mtelela jana Februari 7, 2025. (Na Mpigapicha Wetu)
--------------------------------------
Shule za msingi tatu zilizopo kata ya Iramba wilayani Bunda, mkoa wa Mara zimepokea msaada wa madawati 200 wenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 20 kutoka Benki ya NMB.
Shule hizo ni Mwiruruma iliyopata madawati 100, Buguma na Mumagunga ambazo kila moja ilipata madawati 50.
Makabidhiano ya msaada huo yalifanyika jana Februari 7, 2025 ikiwa ni sehemu ya benki hiyo kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Faraja Ng'ingo alisema ni utaratibu wa benki hiyo kurejesha sehemu ya faida yake kwa jamii.
Ng’ingo alifafanua kuwa baada ya kupokea maombi kutoka kwenye shule hizo, uongozi wa benki hiyo uliona una wajibu wa kutoa msaada huo ukiamini utakuwa na matokeo chanya katika sekta ya elimu wilayani humo.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Salumu Mtelela aliishukuru Benki ya NMB kwa misaada mbalimbali inayoitoa wilayani Bunda, hasa katika sekta za elimu na afya.
Mtelela alitumia nafasi hiyo pia kutuma wito kwa wadau wengine kuiga mfano wa Benki ya NMB katika kuchangia maendeleo ya elimu.
Alisema mazingira bora ya elimu ni moja ya vipaumbele vya serikali, hivyo ushirikiano wa wadau ni muhimu ili kuweza kuboresha sekta hiyo kwa maslahi mapana ya jamii na taifa kwa ujumla.
Naye Kaimu Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Phinias Ouko aliishukuru NMB akisema msaada wa madawati 100 kwa Shule ya Msingi Mwiruruma umemaliza changamoto iliyokuwepo.
Mdau wa elimu ambaye pia ni Katibu wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Dkt Bwire Masinde alisema msaada huo utakuwa na manufaa makubwa kwa watoto wa kata ya Iramba.
Masinde aliwahimiza wakazi wa kijiji cha Mwiruruma kuanza ujenzi wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu huku akiahidi kuunga mkono jitihada hizo ili kupunguza tatizo la upungufu wa majengo hayo katika shule hiyo.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>TANAPA washauriwa kujipanga kuepusha ajali za wanyamapori kugongwa na magari Nyatwali
>>Rais wa zamani wa Namibia Sam Nujoma aaga dunia
>>Nyambari Nyangwine Foundation yaendelea kusambaza msaada wa vitabu sekondari za Tarime Vijijini
>>HABARI PICHA:Wasira kuzuru wilaya za Rorya, Tarime na Serengeti
No comments:
Post a Comment