NEWS

Saturday, 1 February 2025

Mkutano Mkuu WAMACU wapitisha ununuzi kiwanda cha chai, RC awapongeza kwa kuitangaza kahawa ya Arabica



Sehemu ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 15 wa WAMACU Ltd wakifuatilia mada katika mkutano huo mjini Tarime, Mara jana Januari 31, 2025.
---------------------------------

Na Joseph Maunya/ Mara Online News

Mkutano Mkuu wa 15 wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd) umepitisha azimio la ununuzi wa kiwanda cha chai cha ushirika huo.

Mkutano huo ulifanyika mjini Tarime jana Januari 31, 2025 ambapo Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi kama mgeni rasmi.

Meneja Mkuu (GM) wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye alisema kwamba mbali na mazao ya kahawa na chai, ushirika huo unakusudia kupanua wigo kwa kuelekeza nguvu pia kwenye mazao ya mkakati ya alizeti na tumbaku.

GM Gisiboye akizungumza 
katika mkutano huo.
-------------------------------------

GM Gisiboye alisema ushirika huo unajivunia mafanikio makubwa, ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya wanachama, kuingia mkataba wa kuzalisha na kusambaza mbegu za kilimo na serikali kupitia kwa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na kupata hati safi kutoka kwa Mkaguzi kutoka COASCO.

Kwa upande wake mwakilishi wa mgeni rasmi Meja Gowele aliupongeza ushirika wa WAMACU Ltd kwa kazi kubwa ya kuitangaza vizuri kahawa aina ya Arabica inayolimwa Tarime.

“Mnafanya kazi kubwa sana katika kuitangaza kahawa yetu ya Tarime, na kupitia jitihada hizo imekuwa ikipata sifa na ushindi katika mashindano mbalimbali, hongereni sana,” alisema Meja Gowele.

Mwenyekiti wa Bodi ya WAMACU Ltd, Momanyi Range (kulia mbele), Mrajis Msaidizi, Hilda Boniface (katikati) na Meja Gowele wakisalimiana katika mkutano huo. (Picha zote na Mara Online News)
-----------------------------------

Aidha, Meja Gowele aliwahamasisha wanachama wa ushirika huo kuimarisha uzalishaji wa mazao wenye tija, kupeleka kahawa katika kiwanda cha WAMACU Ltd na kudhibiti utoroshaji wa tumbaku kwenda nje ya nchi.

Kwa upande wake Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mwanza, Hilda Boniface aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Mrajis Mkuu na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) akisema ofisi hizo zinajivunia jitihada kubwa zinazofanywa na WAMACU Ltd katika kuchochea maendeleo ya kilimo nchini.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages