
Charles Kajege
Na Mwandishi Wetu, Musoma
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi jana alimwagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo, Gerald Kusaya kufuatilia ili kujua aliko Mbunge wa Mwibara wilayani Bunda, Charles Kajege kwani amekuwa mtoro wa muda mrefu kwenye vikao muhimu vya maendeleo ya wananchi.
Akizungumza katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara kilichofanyika mjini Musoma, Kanali Mtambi alisema mbunge huyo hajaonekana kwenye vikao vya mkoa vinavyojadili maendeleo ya wananchi kwa mwaka mzima sasa.
“Mheshimiwa Kajege, sijui yuko mkoa gani, mwaka mzima. Kuna wabunge hapa zaidi ya mara kumi wamekuja kwa masuala ya wananchi, tunazungumza, tunajadiliana, tunashauri na tunakimbiza masuala ya wananchi, lakini mwaka mzima, eee! Au anaumwa?” alihoji Kanali Mtambi na kuagiza atafutwe:
“RAS (Katibu Tawala wa Mkoa) hebu jaribu kufuatilia tujue mheshimiwa mbunge ana tatizo gani ili tuone kama taratibu zinaturuhusu wakati wa vikao muhimu hivi ambavyo wananchi wanahitaji uwakilishi tuone namna ya jimbo hilo kuwa na uwakilishi badala ya yeye, kwa sababu sasa wananchi wanawakilishwa na nani kwenye jimbo hilo.”
Aidha, Mkuu wa Mkoa aliuomba uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa kuisaidia serikali kumtafuta Kajege huku akisisitiza umuhimu wa wabunge kuzingatia wajibu wao wa kuwakilisha wananchi kwenye vikao vya maamuzi ya kimaendeleo.
“Mwenyekiti wa Chama mtusaidie mambo haya, na niendelee kusisitiza kuwa kazi ya mwakilishi ni kuwakilisha wananchi katika vikao hivi vya kimaamuzi na kisheria, wengine tumejadiliana mambo ambayo wanahitaji yafanyike kwenye majimbo yao, lakini huyo [Kajege] mwaka mzima haonekani,” alisema Kanali Mtambi.
Mara Online News inaendelea na juhudi za kumpata Mbunge Kajege kwa ajili ya kupata kauli yake kuhusu suala hilo.
No comments:
Post a Comment