
Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia Bunge jijini Dodoma leo Novemba 14, 2025.
Dodoma
-------------
Serikali imeunda Tume itakayochunguza kiini cha vurugu na mauaji ya watu yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 29, 2025.
Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo wakati akilituhutubia Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma leo Novemba 14, 2025.
“Serikali imechukua hatua hiyo ili tujue kiini cha tatizo. Taarifa hiyo itatuongoza kujielekeza kwenye mazungumzo ya kuleta maelewano na amani," ameeleza.
Hata hivyo, Rais Samia hakueleza muundo wa Tume hiyo wala muda iliyopewa kukamilisha kazi hiyo.
Amesema amehuzunishwa na matukio ya vurugu na mauaji ya watu - wengi wao wakiwa vijana katika taifa ambalo dunia imekuwa ikijua ni kisiwa cha amani na mfano wa kuigwa.
Vurugu wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu zilitokea katika baadhi ya miji nchini, ambapo Dar es Salaam inadaiwa kuongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha na uharibifu wa mali.
Mpaka sasa jumuiya ya kimataifa bado inaitazama Tanzania kwa umakini kuona hatua itakazochukua katika kuleta maridhiano na ujenzi wa umoja wa kitaifa.
No comments:
Post a Comment