NEWS

Thursday, 3 September 2026

Rais Samia awataka wakuu wa mikoa aliowateua watatue matatizo ya wananchi



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akimuapisha Jumanne Abdallah Sagini kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, katika hafla iliyofanyika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, Septemba 2, 2026.

Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
---------------

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wapya aliowateua, hususan wakuu wa mikoa, kuhakikisha matatizo ya wananchi katika maeneo yao yanapatiwa ufumbuzi.

Rais samia alitoa maelekezo hayo mara baada ya kuwaapisha viongozi hao katika hafla iliyofanyika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, Septemba 2, 2026.

Aliwataka wakuu wa mikoa na wasaidizi wao kutambua kuwa wanakwenda kumwakilisha na kutumikia wananchi, si kujenga mamlaka binafsi.

“Kikatiba Rais amekasimu madaraka yake katika eneo lililokatwa linaloitwa mkoa. Nawe Mkuu wa Mkoa jichukulie kama ndio Rais wa eneo lile, kwamba yote yanayokuja kwa Rais katika eneo hilo, ni ya kwako,” alisema.

Aliwakumbusha viongozi hao kuwa dhamana waliyopewa si ya kuwa wafalme wa maeneo wanayoyaongoza, bali ni ya kuwa watumishi wa wananchi.

“Hatujawapeleka kuwa wafalme wa maeneo hayo, bali kuwa watumishi wa kutumikia watu,” alisema Rais Samia.

Hivyo, aliwataka viongozi hao kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo, uwajibikaji na kujali maslahi ya wananchi.

Wakuu wa mikoa wapya waliapishwa katika hafla hiyo na mikoa waliyopangiwa ikiwa kwenye mabano ni Stanslaus Haroon Nyongo (Pwani) na Alexander Pastory Mnyeti (Geita).

Wengine ni Jumanne Abdallah Sagini (Mbeya) na CP Salum Rashid Hamduni (Mwanza). Naye Richard Kayombo aliapishwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani.

Viongozi walioapishwa katika hafla hiyo wakila kiapo cha maadili ya utumishi wa umma

Rais Samia akiwa katika picha na viongozi mbalimbali wakati wa hafla. (Picha zote na Ikulu)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages