
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Mark Njera.
Tarime
------------
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya limekamata watu 194 kwa tuhuma za makosa mbalimbali, wakiwemo waliokutwa wakiwa na vipande 22 vya nyamapori kavu vyenye uzito wa kilo 24.
Taarifa iliyotolewa juzi Jumapili, Oktoba 25, 2026 na jeshi hilo ilieleza kuwa watuhumiwa wengine ni wa makosa ya kufanya biashara ya dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi.
Makosa mengine ni ya biashara ya pombe haramu ya gongo, kukutwa na nyavu haramu za uvuvi na pikipiki zinazodhaniwa ni za wizi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watuhumiwa hao walikamatwa katika msako kabambe ulioendeshwa na Jeshi la Polisi mwezi huu.
"Jeshi la Polisi limeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia mikutano 272 iliyofanyika katika shule za msingi, sekondari, vyuo, vituo vya waendesha pikipiki, stendi za mabasi, minada, vituo vya redio na kampeni ya Ongea na Kamanda,” ilieleza taarifa hiyo.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment