
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mji wa Serikali wa Mtumba jijini Dodoma jana Ijumaa. Kulia kwake ni Rais wa Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço na kushoto kwake ni Makamu wa Rais, Deogratius John Ndejembi, miongoni mwa viongozi wengine.
Dodoma
--------------
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiambatana na mgeni wake, Rais wa Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço, jana Ijumaa, Oktoba 30, 2026 alizindua rasmi Mji wa Serikali wa Mtumba jijini Dodoma.
Uzinduzi wa mji huo unahitimisha kukamilishwa kwa ujenzi wa majengo 18 ya ofisi za serikali na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 51.2.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, majengo ya ofisi za wizara mbalimbali na taasisi za serkali yatakuwa na uwezo wa kutumiwa na watumishi zaidi ya 18,000.
Mradi wa ujenzi wa mji huo ulibuniwa rasmi tangu mwaka 2016 pale Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli, alipoanzisha kampeni ya "Hamia Dodoma" baada ya kulegalega kwa utekelezaji wa azimio la mwaka 1973 la Halmashauri Kuu ya chama tawala cha TANU wakati huo la kuhamisha makao makuu ya serikali kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Dodoma, katikati ya nchi.

Wazo la kuhamia Dodoma chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, lilipata msukumo mkubwa baada ya Rais wa Awamu Tano, Dkt. John Pombe Magufuli, kuingia madarakani Novemba 2015.
Rais Magufuli alizindua majengo ya kujishikiza ya ofisi za wizara na taasisi za serikali jijini Dodoma mwaka 2019.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Mji wa Serikali wa Mtumba jana Ijumaa, Rais Samia alisifu mifumo ya teknolojia iliyowekwa kwenye majengo yote ya serikali ili kurahisisha mawasiliano na maeneo mengine nchini.
Alisema serikali itajitahidi kuhakikisha mji wa Dodoma unakuwa tofauti na miji mingine kwa miundombinu, utunzaji wa mpango wa jiji na mazingira, uwepo wa huduma muhimu kama vile maji, umeme na nyinginezo.
Rais Samia alitamka kwamba barabara moja ya mji wa Mtumba kwenye ofisi za mabalozi itaitwa Dkt. Antonio Agostinho Neto kwa heshima ya Rais huyo wa Kwanza wa Angola, baada Rais Lourenco kuwa shuhuda wa sherehe ya uzinduzi wake.
No comments:
Post a Comment