NEWS

Thursday, 29 October 2026

Tarime: Wanavijiji, Hifadhi ya Serengeti waazimia kuhuisha ujirani mwema



Mkuu wa Kanda ya Kaskazini Serengeti, Mhifadhi Ezron Lema, akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kegonga, kata ya Nyanungu wilayani Tarime juzi.

Na Christopher Gamaina
Tarime
--------------

Wanavijiji katika kata za Nyanungu, Gorong’a na Kwihancha wilayani Tarime, wamekubaliana na Hifadhi ya Taifa Serengeti, kurejesha uhusiano na ujirani mwema, kwa maendeleo endelevu ya jamii, uhifadhi na utalii.

Makubaliano hayo yalifikiwa kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika kwa nyakati tofauti juzi na jana katika kata hizo, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele.

Kabla ya maazimio hayo, wanavijiji walipewa nafasi ya kueleza kero, changamoto na maoni yao mbele ya Mkuu wa Wilaya na wahifadhi kutoka Hifadhi ya Serengeti.

Miongoni mwa changamoto zilizotajwa na wananchi ni uvamizi wa tembo wanaoharibu mazao mashambani na kutishia usalama wao vijijini.

Aidha, walidai kutopewa fursa za ajira na biashara zinazopatikana ndani ya hifadhi hiyo ili kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.

“Sisi wananchi tuko tayari kwa mahusiano, ila tunaomba hifadhi itusaidie kuboresha huduma za kijamii, vijana wetu wapewe nafazi za kazi hifadhini na wahifadhi wadhibiti tembo wanaotuvamia vijijini,” alisema mkazi wa kata ya Gorong’a, Anatory Chacha Range.

Mwananchi akimweleza Mkuu wa Wilaya Meja Gowele changamoto zinazowakabili wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kegonga katani Nyanungu

Changamoto nyingine iliyotajwa na wanavijiji hao ni upungufu wa maeneo ya kuchunga mifugo unaowalazimu baadhi ya wafugaji kuingiza mifugo ndani ya hifadhi kutafuta malisho na maji.

Walisema hali hiyo husababisha kukamatwa na kutozwa faini, huku baadhi yao wakidai kukumbana na vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu kutoka kwa baadhi ya askari wa hifadhi.

“Wananchi wanalazimika kwenda kunywesha mifugo maji ndani ya hifadhi kutokana na ukosefu wa malambo katika maeneo yetu,” alisema mkazi wa kijiji cha Gibaso katani Kwihancha, Marwa Mhagachi.

Kutokana na hali hiyo, waliiomba serikali na Hifadhi ya Serengeti kuwasaidia kutatua changamoto hizo, huku wakiahidi ushirikiano katika ulinzi wa rasilimali za hifadhi hiyo.

“Tunaomba vijana wetu wapewe fursa za ajira na biashara hifadhini, na tembo wadhibitiwe wasiingie vijijini kuharibu mazao mashambani na kuhatarisha usalama wa wananchi,” alisema Mwenyekiti wa Kijiji cha Karakatonga katani Kwihancha, Amos Waisahi.

Sehemu ya wananchi wakiwa kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Gibaso katani Kwihancha

Kwa upande wao, wahifadhi walisema hifadhi hiyo iko tayari kuendelea kushirikiana na wananchi hao katika utatuzi wa changamoto zao na kuwaelimisha kuhusu manufaa ya uhifadhi kwa jamii na taifa.

Kuhusu tembo wanaoingia vijijini na askari wa hifadhi wasio waadilifu, Mkuu wa Kanda ya Kaskazini Serengeti, Mhifadhi Ezron Lema, aliwaomba wananchi kutosita kutoa taarifa mara wanapoona hali hiyo ili hatua zichukuliwe haraka.

Kwa upande wake Mkuu wa Ulinzi Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mhifadhi Elisamehe Ayubu, alisema: “Tuko tayari kushirikiana na jamii. Uhalifu ukipungua, fedha zinazotumika kugharimia shughuli za ulinzi zitaelekezwa kwenye miradi ya jamii.”

Mhifadhi Ayubu akizungumza kwenye mkutano wa hadhara kijijini Gibaso

Naye Afisa Mahusiano ya Jamii wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mhifadhi Abed Mwesigwa, alisema Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linaendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya jamii katika vijiji hivyo.

“Lakini pia, sisi kama Hifadhi ya Serengeti tuko tayari kuwafamisha wananchi wa maeneo haya fursa za kazi na biashara zinazopatikana ndani ya hifadhi na namna ya kuzipata,” alisema Mhifadhi Mwesigwa.

Mhifadhi Mwesigwa akizungumza katika mkutano wa hadhara kijijini Gibaso

Akihitimisha majadiliano katika mikutano hiyo, Mkuu wa Wilaya, Meja Gowele, aliwataka wahifadhi kuhakikisha wanakutana na wakazi wa vijiji hivyo kila baada ya miezi mitatu kwa majadiliano ya kuimarisha ujirani mwema.

Alisema vikao hivyo vitawapa fursa ya kujadili changamoto zinazojitokeza pande zote na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzitatua kabla ya kuathiri uhusiano baina yao.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akihutubia mkutano wa hadhara kijijini Gibaso. (Picha zote na Mara Online News)

Meja Gowele alisema uhifadhi unahitaji ushirikiano, hivyo wananchi hao wanapaswa kuheshimu sheria na mipaka ya hifadhi hiyo, kujiepusha na vitendo vya ujangili kama vile uwindaji haramu na kuingiza mifugo hifadhini.

“Lengo letu tunataka muishi kwa kushirikiana na kutegemeana, muwe na mahusiano mazuri. Hatutaki watu waishi kwa manung’uniko ndani ya nchi yao,” alisisitiza Meja Gowele.

Kuhusu mvutano wa mpaka wa vijiji na hifadhi hiyo, Mkuu huyo wa wilaya aliwataka kuwa watulivu na wavumilivu wakati wakisubiri maelekezo viongozi wa ngazi ya juu serikalini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages