NEWS

Saturday, 17 October 2026

Waziri Kijaji: Maandalizi ya uzinduzi wa Uwanja wa Gofu Serengeti yamekamilika



Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Gofu Serengeti, leo Jumamosi, Oktoba 17, 2026. (Picha na Mara Online News)

Na Christopher Gamaina
Serengeti
----------------

Maandalizi ya uzinduzi rasmi wa Uwanja wa Gofu uliojengwa pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti katika eneo la Fort Ikoma mkoani Mara yamekamilika, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema.

Waziri Kijaji amethibitisha kukamilika kwa maandalizi hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja huo leo Jumamosi, Oktoba 17, 2026.

Amesema uzinduzi rasmi wa uwanja huo wa gofu utafanyika kesho Jumapili, Oktoba 18, 2026 na kwamba mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ujenzi wa uwanja huo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia kwa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Wizara kuhakikisha zinatangaza zaidi vivutio vya utalii vya asili, sambamba na kubuni vivutio vipya visivyo vya asili ili kuongeza ushindani wa Tanzania katika sekta ya utalii kwenye soko la kimataifa.

“Hiki ndicho kivutio cha utalii cha kwanza pembezoni mwa hifadhi nchini kisicho cha asili,” amesema Waziri Kijaji.

Kwa mujibu wa Waziri Kijaji, hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kupanua wigo wa mazao ya utalii, kuongeza mvuto wa maeneo ya hifadhi na kuvutia watalii wa ndani na wa kimataifa kupitia uzoefu unaounganisha michezo na uhifadhi wa wanyamapori na mazingira ya asili.

Uwanja wa Gofu Hifadhi ya Taifa Serengeti ni kivutio cha kwanza kisicho cha asili kubuniwa na TANAPA ili kuongeza thamani ya vivutio vilivyopo na kuwashawishi zaidi wageni kutembelea Tanzania.

Akielezea upekee wa uwanja huo, Waziri Kijaji amesema wageni watakaokwenda kucheza gofu watapata faida mbili; kwanza, fursa ya kucheza gofu, na pili, kufurahia utazamaji wa wanyamapori na mandari ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages