NEWS

Sunday 4 February 2024

Rais Geingob wa Namibia afariki dunia, Rais Samia atuma salamu za rambirambiHage Geingob
------------------------

RAIS wa Namibia, Hage Geingob (82), amefariki dunia wakati akipata matibabu hospitalini katika mji mkuu wa nchi hiyo, Windhoek.

Makamu wa Rais, Nangolo Mbumba ametangaza kuwa Geingob ameaga dunia alfajiri ya leo Jumapili.

"Mkewe Monica Geingos na wanawe walikuwa karibu naye," Mbumba amesema katika taarifa yake.

Rais Geingob aligunduliwa kuugua saratani na alitangaza hali yake mbele ya umma mwezi uliopita.

Ofisi yake ilitangaza kwamba angesafiri kuelekea Marekani kupata matibabu, na kwamba angerudi Namibia Februari 2, 2024.

Geingob aliapishwa kuwa Rais wa Namibia mwaka 2015, na alikuwa anatumikia awamu yake ya pili na ya mwisho madarakani.

Alifanyiwa upasuaji wa moyo mwaka jana. Namibia inatarajiwa kuandaa uchaguzi mkuu Novemba 2024.

Chama tawala cha Swapo ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 1990, kimemteua Nandi-Ndaitwah kama mgombea urais.

Nandi-Ndaitwah ndiye Waziri Mkuu wa sasa na iwapo atashinda, atakuwa rais wa kwanza mwanamke nchini humo.

Tayari baadhi wa viongozi barani Afrika wakiwemo marais wa mataifa mbalimbvali wameanza kutuma salamu za rambirambi kwa taifa la Namibia na familia ya marehemu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa viongozi hao, ambapo katika ujumbe wa rambirambi uliochapishwa kwenye mtandao wa x [zamani Twitter], amemuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Geingob mahali pema peponi.

Kwa upande wake Rais wa Kenya, Dkt William Ruto amesema Rais Geingob alikuwa kiongozi mashuhuri aliyetumikia watu wa Namibia kwa umakini na kujitolea.

Katika ujumbe wake kwa mtandao wa x, Rais Ruto amesema kiongozi huyo alikuwa muumini wa Afrika iliyounganishwa na alikuza sana sauti na mwonekano wa bara hili katika nyanja ya kimataifa.

Amemuomba Mungu awape nguvu na ujasiri wananchi wa Namibia katika kipindi hiki kigumu. BBC

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages