NEWS

Sunday, 1 February 2026

Waziri Mkuu atembelea Hifadhi ya Arusha,Aipongeza TANAPA




Na Mwandishi Wetu
Arusha
......................................

Waziri wa Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba(Mb), juzi Januari 31, 2026 ametembelea Hifadhi ya Taifa Arusha na kufanya “Amazing Tanzania Tour” kwa lengo la kujionea vivutio vya utalii vilivyopo katika hifadhi hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii wa Tanzania ndani na nje ya nchi.


Katika ziara hiyo, Mhe. Dkt. Nchemba alipokelewa na Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii inayoongozwa na Waziri wake, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), pamoja na viongozi wa Menejimenti ya TANAPA, ambapo alipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya hifadhi yakiwemo vivutio vya wanyamapori, maporomoko ya maji (Tululusia) pamoja na mandhari ya kuvutia ya Mlima Meru uliopambwa na uoto wa asili.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Dkt. Nchemba aliipongeza TANAPA kwa kazi kubwa ya uhifadhi wa maliasili pamoja na ubunifu katika kuendeleza mazao ya utalii, akisisitiza kuwa juhudi hizo zimeendelea kuongeza thamani ya hifadhi na kuvutia wawekezaji na watalii kutoka ndani na nje ya nchi. “Nimejionea kazi nzuri inayofanywa na TANAPA katika kulinda rasilimali zetu na kubuni bidhaa mpya za utalii. Hili ni jambo la kujivunia na lina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa,” alisema.

Aidha, alieleza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta ya utalii ili kuongeza mapato ya nchi na ajira kwa wananchi, huku akihimiza Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika maeneo ya hifadhi za taifa, kutembelea vivutio, pamoja na kulinda urithi huo usiharibiwe kwa manufaa ya sasa na ya baadae.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alisema ziara hiyo ni ishara ya dhamira ya dhati ya Serikali katika kuendelea kuitangaza Tanzania kama kituo bora cha utalii duniani. “Tunamshukuru Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kutenga muda wake kutembelea Hifadhi ya Taifa Arusha. Ziara hii inaongeza hamasa ya kuendelea kuboresha bidhaa za utalii na kuvutia wawekezaji zaidi,” alisema Dkt. Kijaji.

Aliongeza kuwa Wizara, kwa kushirikiana na TANAPA, itaendelea kuimarisha miundombinu ya utalii, huduma kwa wageni na mikakati ya masoko ili kuhakikisha vivutio vya Tanzania vinaendelea kung’ara kimataifa, huku Hifadhi ya Taifa Arusha ikiendelea kuwa miongoni mwa maeneo muhimu yanayochangia kukuza sekta ya utalii nchini

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages