NEWS

Sunday 25 October 2020

Wataalamu wathibitisha ubora wa maji mto Mara

Wataalamu wakichukua sampuli kwenye chanzo cha maji kilichochafuliwa na kemikali kutoka mgodi wa wachimbaji wadogo katika Bonde la Mto Mara kwa ajili ya kupima ubora wake


WATAALAMU wamethibitisha kuwa maji ya mto Mara uliopo mkoani Mara, Tanzania kwa sasa yana ubora unaokubalika kitaifa baada ya changamoto zilizojitokeza katika miezi ya karibuni.

 

Afisa wa Dakio la Mara Mori, Mhandisi Mwita Mataro ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu juzi kwamba vipimo vilivyochukuliwa na wataalamu hivi karibuni vilionesha kuwa kiwango cha ubora wa maji ya mto huo kimeendelea kuongezeka.

Sehemu ya mto Mara

 

Bonde la mto Mara ambao hutiririsha maji katika Ziwa Victoria limekuwa likisongwa na shughuli za uchimbaji madini kwenye baadhi ya ikolojia yake.

 

Shughuli za utafutaji madini katika baadhi ya maeneo zimekuwa zikisababisha uchafuzi ukiwemo wa kutiririsha kemikali kwenda kwenye vyanzo vya maji katika bonde hilo, hivyo kuhatarisha afya na maisha ya viumbe hai ikiwemo mifugo.

Wachimbaji wadogo wa madini wakiwa kazini

 

Aprili 2020, liliripotiwa tukio la ng’ombe 34 waliokufa baada ya kunywa maji yenye kemikali zilizotiririka kutoka mgodi unaomilikiwa na wachimbaji wadogo katika eneo la Nyamongo lililopo ukanda wa Bonde la Mto Mara.

 

Kwa mujibu wa mkazi wa Nyamongo, Augustino Sasi, wananchi wanaoishi ukanda wa Bonde la mto Mara wamekuwa wakihofia usalama wa vyanzo vya maji vilivyo jirani na migodi ya madini.

Wataalamu wakiendelea na shughuli ya uchukuaji sampuli kwenye chanzo cha maji kilichochafuliwa na kemikali kutoka mgodi wa wachimbaji wadaogo katika Bonde la Mto Mara kwa ajili ya kupima ubora wake

 

Naye Bertha Mwita ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Tigite Chini katika Bonde la mto Mara, amesema kumekuwepo na changamoto ya udhibiti wa kemikali za migodini kuingia kwenye vyanzo vya maji.

 

Katika mazungumzo hayo, Sasi na Mwita wamevipongeza vyombo vya habari kwa kazi nzuri ya kuripoti changamoto za mto Mara na vyanzo vyake jambo ambalo limekuwa likisaidia kuzisukuma mamlaka husika kuchukua hatua za ufumbuzi.

 

Aidha, wametumia nafasi hiyo pia kuiomba serikali kupitia wataalamu husika kuendelea kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuhakikisha mto Mara na vyanzo vyake havichafuliwi kwa namna yoyote ile.

 

“Serikali ndio tegemeo letu kubwa katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii, tunaomba iongeze ufuatiliaji na usimamizi wa karibu ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji madini haziathiri ubora na usalama wa vyanzo vya maji ukiwamo mto Mara,” amesema Sasi.

 

Mhandisi Mataro ameunga mkono ushauri huo akisema usimamizi madhubuti wa usalama wa mto Mara unahitajika kwa ajili ya usalama wa afya na maisha ya watu na viumbe hai wengine.

Sehemu nyinyine ya mto Mara


 

Mto Mara unaanzia katika chemchem ya Enapuyapui iliyopo kwenye misitu ya milima ya Mau ambapo maji ya mto huo hutiririka kupitia Hifadhi ya Taifa ya Maasai-Mara nchini Kenya na hatimaye katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tanzania kabla ya kumwaga maji yake kwenye Ziwa Victoria lililounganisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages