NEWS

Tuesday 19 January 2021

Umuhimu wa mboga za majani kwa mjamzito

Mjamzito

UJAUZITO ni kipindi cha miezi tisa toka mimba ilipotungwa hadi wakati wa mama mjamzito kujifungua. Kipindi hiki huambatana na mabadiliko katika mifumo ya mwili ya mjamzito hata kimwonekano.

 

Kipindi cha ujauzito hugawanywa katika vipindi vya miezi mitatu mitatu hadi ukomo wa miezi tisa. Kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ni cha maangalizi ya karibu sana maana huambatana na changamoto nyingi za utokaji wa mimba ulio tatizo siku za hivi karibuni.

Mama mjamzito

Kipindi cha pili ni miezi mitatu mingine na kipindi cha miezi mitatu ya mwisho huwa na matarajio ya kujifungua na maamuzi kufanyika njia ya kujifungua kutokana na changamoto zozote zilizogunduliwa miezi iliyopita, au mahudhurio yaliyopita.

 

Mwanamke huweza kuwa mjamzito pale anapokosa kuona mizunguko yake toka tarehe ya mwisho aliyopata hedhi akiambatana na mabadiliko au maudhi kama kichefu, kutapika, maumivu chini ya tumbo na uthibitisho wa kithibitisha mimba kuonesha majibu kuwa ni mjamzito.

 

Kipindi hiki huleta mabadiliko ya kimwonekano ya mjamzito kuongezeka maziwa na kuchomachoma, chuchu kuwa nyeusi, utokeaji wa mstari mweusi kutoka kitovuni na kushuka hadi sehemu ya chini ya sehemu za siri, tumbo kuanza kuwa kubwa kutokea chini kuja juu na miitikio ya mtoto kuruka.  

Mstari mweusi kutoka kitovuni ni miongoni mwa dalili za ujauzito

Mwanamke aonapo hizi dalili na kuthibitika ni mjamzito basi kuanzia miezi mitatu au minne hupaswa kuanza mahudhurio ya kliniki katika maandalizi na maangalizi ya afya ya mama na mtoto aliye tumboni.

 

Hiki ni kipindi ambacho mama mjamzito hupaswa kuwa na maangalizi ya karibu ya maendeleo yake na mtoto kupitia mahudhurio ya kliniki za mama na mtoto.

 

Mahudhurio haya ya kliniki ni muhimu kwa mama katika kujua au kugundua dalili za hatari za ujauzito kwa matatizo kama kifafa cha mimba, kujua kundi la damu, wingi wa damu, utumiaji wa dawa kinga za Malaria, dawa za minyoo, chanjo, ujuaji wa mlalo, mkao wa mtoto na umri wa mimba.

Ni muhimu mjamzito kuhudhuria kliniki kwa uangalizi wa karibu wa mimba na afya yake 

Pia mahudhurio haya huweza kugundua maambukizi ya magonjwa ya zinaa na maambukizi ya virusi vya ukimwi ili ikiwa pana shida ya kiafya iliyogundulika isimamiwe vizuri kulinda afya ya mama na mtoto.

 

Vifo vya mama na mtoto vinaweza kuzuilika endapo baadhi ya matatizo mengine kama upungufu wa damu kubainika mapema na mama kuhudumiwa kwa ukaribu.

Vifo vya mama na mtoto vinaepukika

Huduma za mama na mtoto zipo katika ngazi mbalimbali za utoaji huduma za afya kuanzia zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, mikoa hadi hospitali za rufaa nchini Tanzania. Hii yote ni kutambua umuhimu mkubwa ulivyo wa kumlinda na kupunguza matatizo ya kuzuilika ya mjamzito kipindi chote cha mimba hadi tarehe za matarajio ya kujifungua.

 

Moja ya changamoto kubwa niliyoweza kuiona kwa kina mama wajawazito ni upungufu wa damu unaosababishwa au kuhusishwa zaidi na upungufu damu wa madini ya chuma “Iron deficiency anemia” ingawa zipo sababu nyingi za upungufu wa damu. Hili ndilo limenishawishi kuona umuhimu mkubwa wa kuzungumzia umuhimu wa mbogamboga kwa mama mjamzito kusaidia ongezeko la damu, hasa aina hii ya upungufu wa damu.

  

Ulaji wa mboga za majani husaidia ongezeko la damu kwa mjamzito

Mboga za majani zina madini chuma na folic asidi kwa kiasi kikubwa. Madini chuma ni malighafi muhimu katika utengenezaji wa chembechembe hai za damu. Mboga za majani kama matembele, majani ya maboga, mchicha na spinachi zina wingi wa madini chuma na vitamin katika kuongeza wingi wa damu na uimarishaji wa kinga ya mwili ya mama mjamzito.  

 

Mboga za majani huchemshwa kidogo au wengine huandaa juisi iliyochanganywa na vyanzo vingine vya madini chuma kama majani ya rozera, parachichi, mbegu za maboga zilizopondwa vizuri, na kiazi chekundu maarufu kama “Beet Roots”.

Mboga za majani zilizochemshwa

Mama mmoja niliyeonana naye kliniki anasema “Mimi nilipokuwa mjamzito mama yangu alikuwa akiniambia nitumie majani ya parachichi, matembele na jani la limao yalichemshwa pamoja. Nilipoenda mahudhurio ya tarehe nyingine ya kliniki niliona ongezeko kidogo la damu.”

 

Wengi wanapopata elimu ya umuhimu wa mboga za majani inapunguza matatizo mengi ya upungufu wa damu usababishwao na madini chuma pungufu.  Mboga za majani hupatikana katika masoko mbalimbali, bustani pandwa za nyumbani kunakorahisisha mama mjamzito kununua na kuandaa mlo wake.

Mboga za majani

Sambamba na umuhimu wa mboga za majani katika kuwa na madini chuma mengi, pia husaidia folic asidi nyingi inayosaidia kupunguza matatizo ya mgongo wazi kwa watoto.

 

Folic asidi haitengenezwi na mwili moja kwa moja, hivyo huhitajika kupatikana kwa njia ya ulaji wa mboga za majani. Wamama wengi wanaokosa ulaji wa madini haya kwa wingi wanayo hatari ya kupata watoto wenye mgongo wazi.

 

Katika kliniki nyingi wajawazito huhimizwa kuchukua tembe za folic asidi. Tembe za kuongeza damu bado haziwezi kutosheleza kupunguza tatizo hili ikiwa himizo la ulaji wa mboga za majani kwa mama wajawazito halitazingatiwa. Elimu hii ni muhimu sana kuwafikia wajawazito na wanaotarajia kuwa wajawazito ili kuepusha matatizo ya upungufu wa damu na mgongo wazi.

Imeandikwa na Dkt Raymond N Mgeni

+255 676 559 211

raymondpoet@yahoo.com



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages