NEWS

Monday 5 February 2024

Jamii yatakiwa kuacha imani ya meno ya plastiki kwa watoto wadogo, RC Mara ataka tathmini ya udumavu



Kikao cha wadau wa afya kikiendelea mjini Musoma jana.
-----------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Musoma
-----------------------------------------


JAMII imetakiwa kuachana na imani ya uwepo wa meno ya plastiki kwa watoto wadogo, badala yake izingatie kuwapeleka kwenye vituo vya huduma za afya wanapobainika kuwa na matatizo ya kiafya.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa afya kilichofanyika mjini Musoma jana Jumatatu, Daktari Bingwa wa Kinywa na Meno, Dkt Nilla Jackson alisema kitaalamu hakuna meno ya plastiki licha ya dhana hiyo kuwepo miongoni mwa jamii.

Dkt Jackson alisema utafiti uliofanya mkoani Mara umebaini kuwa asilimia 87 ya jamii inaamini kuwepo kwa meno hayo, huku asilimia 55 ikiamini matibabu sahihi ya meno hayo ya plastiki ni kuyang'oa.

"Kinachofanyika pale ni ukatili wa hali ya juu - watoto wanang'olewa meno - tena kwa kutumia vifaa ambavyo sio salama na hawachomwi ganzi wala kufuata taratibu za kimatibabu," alisema.

Kwa mujibu wa Dktari huyo, kuna madhara mengi yanayotokana na ung'oaji huo wa meno, ikiwa ni pamoja na kuharibu mpangilio wa meno, mapengo na hata vifo.

"Kinachoonekana kuwa ni meno ya plastiki ni mbegu za meno, kwa hiyo wakiyang'oa meno hayataota tena. Kinachotakiwa ni kuwapeleka watoto hospitalini kwa ajili ya matibabu sahihi kwani unakuta mtoto anaumwa magonjwa mengine wao wanadhani ana meno ya plastiki, mwisho wake mtoto anapoteza maisha," alisema Dkt Jackson.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt Vicent Naano alisema kuna haja ya kuwajengea wananchi uelewa ili waachane na dhana hiyo ya meno ya plastiki.

"Tatizo ni kubwa katika jamii yetu, nadhani tuje na maamuzi ambapo pamoja na mambo mengine, elimu ianze kutolewa katika vituo vya huduma za afya, hasa wakati wa mahudhurio ya kliniki ya mama na mtoto," alisema Dkt Naano.


Naano akichangia hoja kikaoni
-----------------------------------------
Baadhi ya wakazi wa Musoma waliunga mkono hoja hiyo, wakisema wananchi wakipata elimu wanaweza kuondokana na dhana ya uwepo wa meno ya plastiki.

"Mimi nilimpeleka mtoto wangu kwa mtaalamu akang'olewa na nilifanya hivyo baada ya kuambiwa nikichelewa mtoto atakufa, laiti ningejua kuwa hakuna kitu kama hicho basi mwanangu asingeng'olewa jino," alisema Anna Merengo.

"Wengi wanafanya hivyo kwa sababu hawana elimu, na ni kweli ukiangalia wengi waliong'olewa meno ya plastiki wana mapengo, na wengi hawajui kama shida ilianzia hapo, Sasa ni vema elimu ikatolewa hasa kwa maeneo ya vijijini ili watu wajue madhara ya suala hili," alisema Joyce John.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda ametumia nafasi ya kikao hicho kuziagaza halmashauri zote mkoani humo kufanya tathmini ili kujua hali halisi ya udumavu wa watoto.

Mtanda alifikia hatua hiyo kutokana na kutokuwepo kwa taarifa ya hali ya udumavu katika halmashauri hizo licha ya takwimu kuonesha kuwa tatizo hilo lipo kwa asilimia 23.4.

"Naagiza tathmini ifanyike haraka iwezekanavyo ili tuweze kupanga namna ya kupambana na udumavu katika mkoa wetu kwani ni vigumu kupata matokeo chanya wakati hatuna hali halisi katika halmashauri zetu," alisisitiza.


Mtanda akizungumza kikaoni
---------------------------------------
Ofisa Lishe Mkoa wa Mara, Benson Sanga alisema takwimu za mwaka 2022 zinaonesha kuwa mkoa huo unakabiliwa na udumavu kwa asilimia 23.4, na kwamba ipo mikakati kadhaa inayofanyika ili kuhakikisha tatizo hilo linapata ufumbuzi.

"Tumeanza kuhamisisha programu za uzalishaji wa chakula katika kila shule badala ya kutegemea chakula kinachotolewa na wazazi, na hii itawezesha wanafunzi wote kupata chakula shuleni," alisema Sanga.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages