NEWS

Friday 6 November 2020

Mwenyekiti Chadema Serengeti abwaga manyanga

Francis Muhingira Garatwa


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Francis Muhingira Garatwa, ametangaza kujiuzulu wadhifa huo leo Novemba 6, 2020.


Katika barua yake ya kujiuzulu, Garatwa amesema “Kwa hiari yangu mwenyewe bila kushawishiwa na mtu yeyote yule, nimelazimika kujiuzulu Uenyekiti wa Chama Ngazi ya Wilaya kutokana na aina ya wenzetu tunaofanya nao kazi wanavyotumiwa na maadui zetu kukiumiza chama huku waking’ata na kupuliza.


“Tunatumia muda na jitihada kubwa sana za kila namna katika kukijenga na kukiimaarisha chama hapa wilayani, lakini wasaliti waliomo ndani yetu, wanashiriki kutukwamisha na kuturudisha nyuma kwa kiwango kikubwa sana kwa manufaa yao.


“Katika kipindi chote hiki cha Uchaguzi Mkuu, pamoja na jitihada kubwa tulizofanya kwa kushirikiana na viongozi wenzetu wa ngazi mbalimbali ndani ya chama ili kukivusha chama salama kwenye Uchaguzi, lakini tulikutana na wakati mgumu sana hasa wakati wa michakato ya Uchaguzi ukiachilia mbali matukio yaliyotokea siku husika ya uchaguzi kwa sababu tayari baadhi ya wenzetu walikuwa kazini kuhakikisha tunakwama, hii ilitokana na makubaliano kati yao na maadui zetu tuliokuwa tunapambana nao.


“Pamoja na kwamba hali hii [ya Chadema kushindwa] imetokea kwa nchi nzima, ni vyema pia ukweli ubakie pale pale kwamba, kuna baadhi ya maeneo ikiwemo hapa kwetu, chama kiliumizwa sana wakati wa michakato ya uchaguzi hata kabla ya siku yenyewe ya uchaguzi.


“Hivyo basi, kutokana na hayo niliyoyaeleza hapo juu, nimelazimika kujiuzulu nafasi yangu ya Uenyekiti wa Chama Ngazi ya Wilaya ili kupisha mtu mwingine aendeleze pale nilipoishia,” amesema Garatwa.


Hata hivyo alipoulizwa na Mara Online News kwa njia ya simu leo jioni, Garatwa ambaye alikuwa diwani wa kata ya Nyansurura wilayani Serengeti na mgombea aliyetetea nafasi hiyo kwa tiketi ya Chadema katika Uchaguzi Mkuu uliopita bila mafanikio, amethibitisha kujiuzulu nafasi hiyo, lakini hakuwa tayari kusema iwapo atajiunga na chama kingine cha siasa au la.

(Imeandikwa na Mara Online News)

2 comments:

  1. Ni udhaifu mkubwa kuona ukikimbia majukumu yako kisa jukumbana na adui katika kutimiza wajibu wako. Kimsingi sharti usimame kwa zamu yako kuhakikiasha unakua kiongozi mwema na mairi mwenye kudhibiti kila aina ya dhuruma na adui yeyote anayeingilia uyendaji wako hata kufelisha matarajio chanya. Mr. Una nafasi ya kutafakari upya.

    ReplyDelete
  2. Kimsingi maelezo yako yanaonekana kama yana Mashiko lakin Kumbuka uliapa kukitumikia Chama Leo Unaamua kuacha Kaz eti Kisa wasaliti,Duniani hapa hakuna kaz isiyo na CHANGAMOTO RAFIKI Hata kwetu huku wapo tafakari vizuri Ushaur wangu rudi utumikie Chama

    ReplyDelete

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages