NEWS

Tuesday 26 April 2022

Uongozi CDC wafunguka tuhuma za kutoshirikisha wataalamu miradi ya CSR Barrick North Mara



KAMATI ya Maendeleo ya Jamii (CDC), inayohusisha vijiji 11 vilivyo jirani na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara wilayani Tarime, imesema haijawahi kukwepa kushirikisha wataalamu wa kisekta katika mipango ya miradi ya kijamii.

Mwenyekiti wa CDC hiyo, Paul Bageni (aliyesimama pichani juu) ametoa ufafanuzi huo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Nyamongo juzi.

Bageni alikuwa akijibu tuhuma dhidi ya CDC hiyo zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Hapi, wakati wa kikao cha wadau wa maendeleo, kilichofanyika mjini Musoma, Aprili 20, 2022, ambapo pia kiongozi huyo wa mkoa alitoa tamko la kuivunja kamati hiyo na kuwagiza vyombo vya dola kuchunguza viongozi wake.

RC Hapi alichukua hatua hiyo baada ya Kamati ya Uchunguzi Maalum kuwasilisha kwake ripoti iliyoonesha kuwa CDC hiyo imehusika kwenye ubadhirifu wa sehemu ya shilingi bilioni tano zilizotolewa na mgodi wa North Mara.

Fedha hizo zilitolewa chini ya Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa mwaka 2019, ili kugharimia utekelezaji wa miradi ya kijamii katika vijiji vilivyo jirani na mgodi huo.

Pamoja na mambo mengine, mkuu huyo wa mkoa alidai kuwa CDC hiyo imekuwa haishirikishi wataalamu wa kisekta katika mipango ya utekelezaji wa miradi ya kijamii.

Hata hivyo, Mwenyekiti Bageni amesema CDC hiyo imekuwa ikitekeleza majukumu yake ya kusimamia mipango ya miradi ya kijamii kwa kufuata utaratibu na kushirikisha wadau husika.

“Tumekuwa tukitekeleza majukumu yetu kwa uwazi, kwanza kijiji husika kinaibua mradi, baadaye mpango unapelekwa kwenye mkutano mkuu wa kijiji, kisha kwenye Kamadi ya Maendeleo ya Kata (WDC) husika,” amesema Bageni.

Ameongeza kuwa baada ya hatua hizo, mpango wa miradi hupelekwa kwenye Kamati ya Wakuu wa Idara (CMT) ya Halmashauri, kisha kwenye halmashauri yenyewe - ambayo hupitisha mpango husika, kabla ya kuupeleka ngazi ya mkoa na baadaye wizara husika kupata baraka za utekelezaji.


Baadhi ya wajumbe wa CDC wakifuatilia jambo mkutanoni

“Kwa hiyo, CDC huwa tunapeleka mipango ya miradi ilioibuliwa na wanavijiji kwa wataalamu - maana wao ndio wanajua gharama za miradi,” amesisitiza Bageni.

Ametaja baadhi ya miradi iliyoibuliwa na wanavijiji chini ya usimamizi wa CDC hiyo na kutekelezwa chini ya usimamizi wa wataalamu husika kuwa ni ujenzi wa barabara ya lami mjini Nyamongo na mradi wa maji wa Nyangoto.

Bageni amefafanua kuwa mradi wa ujenzi wa lami Nyamongo ulisanifiwa na utekelezaji wake kusimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA), huku ule wa maji Nyangoto ukisanifiwa na kusimamiwa na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Tarime.

Ameshutumu kitendo cha viongozi na wanachama wa CDC hiyo kutuhumiwa bila kupewa nafasi ya kusikilizwa, huku akisema yuko tayari kuhojiwa dhidi ya tuhuma zinazowakabili.

“Tumechafuliwa, ninasubiri nikamatwe na nitawapa ushirikiano. Mkuu wa Mkoa awe anasikiliza pande zote, yeye ni kiongozi mkubwa, tunamheshimu lakini awe anasikiliza watu wa chini,” amesema Mwenyekiti huyo wa CDC Tarime.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages