NEWS

Monday 20 June 2022

Right to Play, AICT wahamasisha ulinzi wa mtoto na elimu kwa wasichana



Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Rebeca Bugota (kushoto) na viongozi wengine wakikabidhi zawadi za makombe kwa wanafunzi walioshinda mpira wa miguu na pete kwenye tamasha la michezo lililolenga kuhamasisha ulinzi wa mtoto na umuhimu wa elimu kwa wasichana katika Shule ya Msingi Nyantira iliyopo kata ya Nyansincha wilayani Tarime, wiki iliyopita.

SHIRIKA la Right to Play kwa kushirikiana na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, wametumia tamasha la michezo mbalimbali kwa wanafunzi, kuhamasisha ulinzi wa watoto na umuhimu wa elimu kwa wasichana, wakiwemo wenye ulemavu.

Tamasha hilo limefanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Nyantira iliyopo kata ya Nyansincha wilayani Tarime hivi karibuni, likihusisha michezo ya mpira wa miguu na pete.


“Shirika la Right to Play linafanya jitihada nyingi kuhakikisha mtoto anaongeza uwezo wake wa kusoma, na linawapa watoto wote; wa kike, wa kiume na wenye ulemavu fursa sawa ya kupata elimu.

“Kwa hiyo wazazi mliopo hapa wapeni watoto nafasi ya kusoma kwa sababu elimu ndiyo inaweza kuwasaidia watakapokuwa wakubwa wasiwe tegemezi, walifae taifa letu kwa maendeleo,” amesema Rebeca.

Wakati huo huo, Shirika la Right to Play na Kanisa hilo la AICT wameadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu, kwa kuandaa tamasha la michezo, ikiwemo mpira wa miguu, pete na kuvuta kamba kwa wanafunzi wavulana na wasichana katika Shule ya Msingi Gwitare, iliyopo kata ya Nyamwaga wilayani Tarime, ambapo washindi wamepewa zawadi za vikombe na madaftari.


Akizungumza katika tamasha hilo, Rebeca amesema wanashirikiana na Right to Play kuhamasisha masuala ya kielimu kwa wanafunzi wa shule hiyo.

“Hapa Gwitare tunasaidia masuala ya kielimu ili kuona mwamko wa elimu mahali hapa unakuwa mzuri na watoto wanatimiziwa mahitaji yao yote,” amesema.

Ameongeza kuwa wanawasaidia pia watoto kuwa na stadi za maisha kupitia kituo cha usomaji kilichopo Gwitare siku za Jumatano na Ijumaa.



Naye Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Gwitare, Godfrey Denis amesema Shirika la Right to Play limewasaidia mambo mengi, hasa kuelimisha jamii kuepuka ukatili kwa watoto na namna bora ya kuwasaidia katika masomo.

“Tunashukuru tumekuwa nao katika tamasha hili, tumeweza kuelimisha jamii juu ya namna ya kumlinda mtoto na kuangalia haki za mtoto, tunaomba waendelee kuwepo kwa ajili ya kusaidia jamii,” amesema Mwalimu Denis.


Mwalimu Denis (pichani mwenye koti) ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa jamii kuwapa watoto wa kike elimu na kuacha kuwakeketa.

Right to Play ni shirika la kimataifa lililopo Canada, linalosaidia watoto na vijana kujikomboa kutoka kwenye matatizo mbalimbali, na linafanya kazi katika nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania.

Kwa Tarime, linawasaidia watoto, hususan wanaosoma shule za msingi, ili waweze kukuza uwezo wao wa kusoma.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages