
Paul Chacha Makuri
Na Mwandishi Wetu, Serengeti
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Chacha Makuri, ametangaza rasmi nia ya kugombea ubunge wa jimbo la Serengeti mkoani Mara katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Oktoba 2025.
“Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, ninawajulisha rasmi kuwa tarehe 27 Juni 2025, nimesimama mbele ya jamii yangu ya Serengeti na taifa kwa ujumla, kutangaza nia yangu ya kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Serengeti kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 2025,” amesema Makuri katika taarifa yake kwa vyombo vya habari na umma leo Ijumaa.
Hii ni mara ya pili kwa kada huyo kijana wa CCM kujitokeza kuwania ubunge katika jimbo la Serengeti. Mara ya kwanza alijitokeza kuwania nafasi hiyo mwaka 2020 lakini hakufanikiwa.
“Hata hivyo, sikukata tamaa. Niliendelea kujifunza, kujiimarisha, kuwatumikia watu wangu katika nyanja nyingine na kujiandaa kwa bidii zaidi,” amesema Makuri na kuendelea:
“Mwaka huu 2025, baada ya kutafakari, kusikiliza maoni ya watu wangu na kuona fursa ya ujenzi mpya wa taifa letu, nimerudi tena mbele ya chama changu na wananchi kuomba nafasi hii kwa moyo mweupe na nia safi.”
Makuri amesema anaomba ridhaa ya wananchi ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Serengeti ili aweze kurudisha kile alichokiita sauti ya Serengeti kwenye meza ya kitaifa.
“Jimbo letu limekuwa kimya kwa muda mrefu. Tunahitaji mbunge mwenye uwezo wa kuwasilisha hoja zenye mashiko kwa maslahi ya wananchi wetu,” amesema.
Ameongeza kuwa anaomba nafasi hiyo ya ubunge ili kuleta mshikamano wa kweli kwa wana-Serengeti bila kujali tofauti za kabila, koo wala itikadi za kisiasa. “Uzalendo wetu kwa Serengeti unapaswa kuwa juu ya tofauti zetu,” amesisitiza Makuri.
Pia, Makuri amesema akifanikiwa kuwa Mbunge wa Serengeti atasimama imara katika kuchangia utekelezaji wa Ilani ya CCM 2025–2030 ili kuimarisha kazi nzuri ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika jitihada za kuboreshea wananchi huduma za kijamii, ikiwemo afya, elimu, maji, barabara, umeme na utawala bora.
“Vipaumbele vyangu vikuu iwapo nitapata ridhaa ya wananchi ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Serengeti ni miundombinu ya Barabara, ambapo nitapigania kwa nguvu zote ujenzi wa barabara za lami kuunganisha Serengeti na wilaya za jirani za Tarime Bunda na Musoma, kwani usafiri ni injini ya Uchumi,” amesema Makuri.
Kwenye huduma za afya na elimu, amesema atahakikisha huduma hizo zinaboreshwa, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa walimu, watumishi wa afya, vifaa na mazingira bora ya kujifunzia na kuhudumiwa.
Katika masuala ya ajira na uwezeshaji kwa vijana, Makuri amesema ataelekeza nguvu karika uanzisha programu za ujuzi, mafunzo ya kazi na fursa za mitaji kwa vijana kupitia SACCOS, VICOBA na sekta binafsi.
Kuhusu kupambana na umasikini na kuinua uchumi vijijini, amesema ataweka msukumo katika kuhamasisha kilimo cha kisasa, ufugaji wa tija, masoko ya bidhaa na sera wezeshi za kiuchumi kwa wananchi wa kipato cha chini.
“Dira yangu ni kuinua Serengeti kwa Pamoja. Ninajitokeza si kwa kusukumwa na makundi au maslahi binafsi, bali kwa wito wa ndani wa kuwatumikia watu wangu. Nipo tayari kuwa daraja la maendeleo, kusikiliza na kusuluhisha, kushirikiana na kuunganisha – kwa maslahi ya jimbo la Serengeti,” amesisitiza Makuri.
Aidha, Makuri amekiomba chama chake cha CCM wananchi wa Serengeti kwa ujumla kumpokea na kumpa nafasi ya kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
“Pia, naomba wananchi wa Serengeti wanipokee kama mtoto wao, kijana wa kizazi hiki, mzalendo wa kweli na mwenye kiu ya maendeleo ya watu wake. Serengeti yetu. Jamii yetu. Maendeleo yetu. Wakati ni sasa na siku ni leo.
“Kwa pamoja tunaweza kuijenga Serengeti mpya yenye mshikamano, maendeleo na ustawi kwa wote. Naamini ndani ya CCM, na naamini kwa wananchi wa Serengeti. Kazi na Utu, Tunasonga Mbele. Kidumu Chama Cha Mapinduzi,” amehitimisha Paul Chacha Makuri, mtia nia wa nafasi ya ubunge jimbo la Serengeti.
No comments:
Post a Comment