
Na Mwandishi Wetu
Musoma
--------------



Musoma
--------------
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeendesha semina ya siku moja kwa waandishi wa habari wa mkoani Mara kuwajengea uelewa kuhusu majukumu ya mamlaka hiyo na mchango wake katika maendeleo ya sekta za nishati na maji nchini.
Semina hiyo imefanyika leo Jumanne, Juni 23, 2026, mjini Musoma, ambapo wanahabari hao wameelimishwa shughuli za EWURA na huduma zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo.
Miongoni mwa mada zilizowasilishwa katika semina hiyo ni kazi na majukumu ya Ofisi ya EWURA Kanda ya Ziwa, uwekezaji wa vituo vya mafuta vijijini, wajibu wa EWURA katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na jinsi inavyopokea na kutatua malalamiko na migogoro katika sekta zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo.
Wawezeshaji wa mada hizo ni Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Nyirabu Musira, Mkaguzi wa Mafuta Kanda ya Ziwa, Atubele Byamungu na Ofisa Huduma kwa Wateja, Jesca Sewando.
Watoa mada hao wameeleza EWURA inavyoendelea kusimamia kwa karibu utoaji wa huduma bora, salama na endelevu katika sekta za nishati na maji, huku ikihakikisha wananchi wanapata haki zao kupitia mifumo mbalimbali ya usimamizi na utatuzi wa migogoro.
Aidha, semina hiyo imewapa wanahabari hao fursa ya kuuliza maswali, kutoa maoni na kupata ufafanuzi kuhusu changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sekta hizo.

Wawezeshaji na washiriki wa semina hiyo wakifurahia picha ya pamoja.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara, Mugini Jacob, amewashukuru wawezeshaji kwa semina hiyo, akisema imewawezesha kuelewa masuala ya udhibiti wa huduma za nishati na maji.
Jacob amesema maarifa waliyoyapata katika semina hiyo yatawawezesha kuandika habari sahihi kuhusu EWURA na zenye manufaa kwa wananchi.

Jacob akitoa neno la shukrani kwa wawezeshaji wa semina hiyo kutoka EWURA. Kushoto ni Mhandisi Musira na kulia ni Kaimu Katibu wa MRPS, Fresha KInasa.
“Tunawashukuru kwa mafunzo haya muhimu, tunawaahidi kwamba tutakuwa mabalozi wazuri wa EWURA kupitia kalamu zetu kwa kuhabarisha umma kuhusu majukumu na huduma zinazodhibitiwa na mamlaka hii,” alisema Mugini.
Naye mwandishi wa habari kutoka Mara Online News, Christopher Gamaina, amesema semina hiyo ni hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano kati ya EWURA na wanahabari na kuhakikisha umma unapata taarifa sahihi kuhusu huduma zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo kwa maendeleo ya jamii na taifa.

Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Nyirabu Musira (kushoto), akikabidhi zawadi kwa Mwenyekiti wa MRPC, Jacob Mugini, baada ya semina hiyo. (Picha zote na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment