
Mkuu wa Kitengo cha Afrika ya Kati na Mashariki cha Ujerumani, Joachim Schmitt, akikagua zahanati mpya iliyozinduliwa katika kijiji na kata ya Enguserosambu, wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, Agosti 17, 2026.
Ngorongoro
------------------
Zahanati iliyojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Ujerumani kupitia Benki yake ya Maendeleo (KfW), imezinduliwa katika kijiji na kata ya Enguserosambu, wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Uzinduzi huo ulifanyika Agosti 17, 2026 na kushuhudiwa na ujumbe kutoka Serikali ya Ujerumani, Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS), viongozi na wakazi wa maeneo yatakayonufaika na mradi huo wa afya.
Zahanati hiyo mpya ambayo ujenzi wake umegharimu shilingi milioni 540, inatarajiwa kunufaisha wakazi zaidi ya 5,000 kwa kuwaboreshea upatikanaji wa huduma za afya.
Mbali na uzinduzi wa zahanati hiyo, viongozi wa mashirika hayo walitembelea na kukagua mingine minne ya kijamii wilayani Ngorongoro, inayofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia KfW.
Miradi hiyo ni ujenzi wa bwawa la maji katika kata ya Olorieni - Magaiduru unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi zaidi ya bilioni moja, ambao unalenga kutatua changamoto ya maji kwa binadamu na mifugo ili kupunguza migogoro kati ya wafugaji na maeneo ya hifadhi.
Akiwa katika mradi huo wa bwawa, Kiongozi wa ujumbe huo kutoka Serikali ya Ujerumani, Schmitt, alieleza kufurahishwa na mradi huo na kutoa wito kwa jamii na serikali kuutunza kwa ajili vizazi vya sasa na vichavyo.
Miradi mingine iliyotembelewa ni vikundi vya Benki Hifadhi ya Jamii (COCOBA) vinavyonenepesha kondoo kwa ajili ya kipato cha kuendesha maisha yao, maendeleo ya msitu wa asili wa Enguserosambu na maboma ya kijamii, pamoja na kuzungumza nao kuhusu manufaa ya misaada inayotolewa na Ujerumani.
Miradi hiyo inalenga kuboresha maisha ya jamii, kuchagiza na kuimarisha uhifadhi shirikishi katika jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi za wanyamapori.
Kwa mjibu wa Meneja Miradi wa FZS Kanda ya Serengeti, Masegeri Rurai, hiyo ni miongoni mwa miradi 36 ikiwemo ya afya, elimu, maji na barabara inayotekelezwa na TANAPA kwa ufadhili wa Serikali ya Ujerumani, huku FZS wakiwa wawezeshaji.
Mwakilishi wa Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Nuhu Daniel Massay, aliushukuru ujumbe wa Serikali ya Ujerumani, KfW na FZS kwa ushirikiano wanaotoa kwa Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya kijamii.
"Matokeo ya ushirikiano huo kati ya serikali mbili yanaonekana, watoto wanasoma katika vituo bora zaidi, upatikanaji wa huduma za afya, barabara, huduma za masoko na malambo ya maji,” alisema Nuhu na kuongeza:
"Mafanikio haya yanawakilisha zaidi miradi binafsi, yanaonesha thamani ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Ujerumani kuhakikisha uhifadhi unachangia kwa kina maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwenye maeneo yaliyohifadhiwa.”






No comments:
Post a Comment