
Mbunge Mary Daniel Surati
Na Mwandishi Wetu
Tarime
------------
Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mary Daniel Surati (CCM), ameahidi kumpa ofa maalum mwanafunzi bora wa Shule ya Sekondari Manga, Deborah Mussa Robert, kwa kupata ufaulu wa daraja la kwanza la alama nne katika Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mwaka 2026.
Ahadi hiyo ni ya kumjumuisha mwanafunzi huyo kwenye kundi la wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani yao kutoka wilaya ya Serengeti, watakaofanya ziara ya kujifunza katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, kupitia programu ya mbunge huyo ya Samia Uthubutu Award.
Mary alitoa ahadi hiyo wiki iliyopita wakati wa hafla ya kuwapa tuzo wadau wa maendeleo wa Shule ya Sekondari Manga wilayani Tarime, iliyoandaliwa shuleni hapo chini ya uongozi wa Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Editha Lazaro Nakei.
Mbunge huyo kijana alisema Deborah atashiriki ziara hiyo akiwa ameambatana na mwalimu mmoja wa kike kutoka shule yake ili kuhakikisha anapata usimamizi stahiki wakati wa safari hiyo ya mafunzo.
Ziara hiyo inalenga kuwapa wanafunzi hao uelewa kuhusu shughuli za bunge, uongozi na utendaji wa taasisi za serikali, ikiwa pia ni sehemu ya kuwajengea ari ya kuendelea kufanya vizuri katika masomo na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.
Mbunge Mary anatoa ofa hiyo kuonesha kutambua na kuthamini juhudi za wanafunzi wanaofanya vizuri, hali ambayo inahamasisha wanafunzi wengine kujituma kwenye masoma ili waweze kufikia ndoto zao.
Programu ya Samia Uthubutu Award inajenga utamaduni wa kuthamini mafanikio ya kielimu na kuwapa vijana motisha ya kuthubutu, kufanya vizuri na kuamini kwamba juhudi zao zinaweza kufungua milango ya fursa kubwa zaidi katika maisha yao.

Mwanafunzi Deborah Musa Robert akipokea zawadi ya laptop kutoka kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Thobias Elias Ghati, iliyotolewa na uongozi wa Shule ya Sekondari Manga wakati wa hafla hiyo. Aliyeshikilia kipaza sauti ni Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Editha Lazaro Nakei.
No comments:
Post a Comment