NEWS

Friday 24 April 2020

Ajali basi la Zakaria yajeruhi makumi hifadhini SerengetiMAKUMI ya abiria wamejeruhiwa baada ya basi la Zakaria lililokuwa likitokea jijini Arusha kuelekea wilayani Tarime, Mara kupata ajali ya kupinduka ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Misana Mwishawa, ameiambia Mara Online leo Ijumaa kwamba ajali hiyo imetokea jana Aprili 23, 2020 katika eneo la Seronera.

Kwa mujibu wa Mwishawa, basi hilo lilikuwa na abiria 43 na wahudumu watatu na kwamba waliojeruhiwa vibaya ni dereva, kondakta na abiria mmoja wa basi hilo.

                   Massana Mwishawa mkuu wa hifadhi ya Serengeti

“Hao watatu waliojeruhiwa vibaya tulitumia gari letu dogo kuwapatia msaada wa kuwawahisha kwenda kupata matibabu wilayani Bunda kupitia lango letu la Ndabaka baada ya kushindwa kupita kwenye daraja la Grumeti wilayani Serengeti ambalo limefunikwa na maji.

“Majeruhi wengine tumetumia madaktari wetu wa hifadhi kuwapatia matibabu ikiwa ni pamoja na kushona majeraha bila malipo,” amesema Mwishawa.

Amesema abiria wengine wote walipatiwa huduma za maji ya kunywa na malazi kwenye hosteli za hifadhi bila malipo.

“Kwa sasa tunatafuta chombo cha kunyanyua basi hili,” amasema Mhifadhi Mkuu huyo wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Tunaendelea na juhudi za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi juu ya ajali hiyo.

(Habari na Christopher Gamaina)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages