
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi (katikati), akizungumza katika kikao cha kupokea taarifa za maambalizi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 kutoka wilaya za mkoa huo mjini Musoma leo.
------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Musoma
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, leo amepokea taarifa za maandalizi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 kutoka wilaya na halmashauri za mkoa huo, na kuzitaka kuongeza nguvu katika maandalizi ya mbio hizo.
“Angalieni mapungufu ya mwaka jana muone ni maeneo gani yanahitaji kurekebishwa kwa haraka kwa kuzingatia vigezo vya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu,” amesema Kanali Mtambi.
Aidha, amesema kwamba bila maandalizi ya kutosha na kuwataka wakuu wa wilaya kuzisimamia halmashauri zao kikamilifu, huku akiwatahadharisha kuwa uongozi wa mkoa hautakubali kuaibika.
Amewataka wakuu wa wilaya na kamati za usalama za wilaya kutembelea miradi iliyoainishwa na halmashauri mapema, ili kutoa nafasi za maandalizi kukamilika katika miradi itakayokubaliwa.
Kanali Mtambi ameipongeza wilaya ya Butiama kwa kuanza kufanya vikao vya maandalizi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru na kukagua miradi itakayotembelewa na mwenge huo mwaka huu.
Ameipongeza pia taarifa ya maandalizi na mipango ya wilaya ya Serengeti iliyowasilishwa katika kikao hicho kilichofanyika mjini Musima.
Mkuu huyo wa Mkoa ameitaka wilaya ya Musoma kuboresha shughuli za hamasa ya Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 na kumtaka Katibu Tawala wa Mkoa kuitumia Brass Band ya SENAPA katika mapokezi na makabidhiano ya Mwenge huo na kumshirikisha Julius Masubo Kambarage katika maandalizi ya mbio hizo mkoani Mara.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mbio za Mwenge Mkoa wa Mara, Fidel Baragaye, amesema mwaka huu mbio za mwenge zitaingia katika mkoa wa Mara Agosti 15, 2025 kutokea mkoa wa Simiyu na kukimbizwa katika halmashauri zote tisa na kukabidhiwa kwa mkoa wa Mwanza Agosti 24, 2025 katika wilaya ya Ukerewe.
Baragaye amesema kwa mwaka 2025, ukaguzi utakaofanywa na Mwenge wa Uhuru utakwenda sambamba na ukaguzi wa miundombinu ya zamani, utakagua kisayansi kwa kutumia vifaa vya kisasa na mwenge utaenda katika maeneo ambayo hayajapitiwa na Mwenge wa Uhuru.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zilizinduliwa Aprili 2 katika mkoa wa Pwani, na kilele chake ni Siku ya Kumbukumbu ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Wiki ya Vijana Kitaifa Oktoba 14, 2025 katika mkoa wa Mbeya.
Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 inasema: “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu”.
No comments:
Post a Comment