PAMOJA na umuhimu wa Fomu
Namba Tatu ya Polisi (PF3) katika kumsaidia mhanga hasa wakati wa kutoa ushahidi
mahakamani, uelewa, upatikanaji na ujazaji wa fomu hiyo bado ni tatizo
linalohitaji ufumbuzi katika wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Utafiti uliofanywa na Mara
Online News katika wilaya hiyo hivi karibuni umebaini kuwa wananchi wengi wakiwamo
viongozi hawajui PF3, kazi yake, wala inakopatikana.
Mkazi wa kijiji cha
Mwaging’hi, Edna Didas alipoulizwa iwapo anafahamu fomu hiyo amesema “Sijui
PF3. Kwani inapatikana wapi, kazi yake ni nini? Naomba unisaidie niijue.”
Mwanamke huyo amesema ni
mara ya kwanza kusikia kwamba kuna kitu kinachoitwa PF3 na kusisitiza kuwa
hajapata kuona mtu akiwa na fomu hiyo, wala kusikia ikiongelewa na yeyote
kijijini hapo.
Mkazi wa kitongoji cha
Manguluma, Mchungaji Melkisadick John naye amesema hafahamu PF3 na kazi yake.
“Sijui hiyo PF3, sijui kabisa hiyo inahusiana na nini,” amesisitiza huku
akishindwa kuitamka kwa usahihi fomu hiyo.
Naye Mwenyekiti wa
Kitongoji cha Luzela, Musa Malole, amesema “Sifahamu PF3, sijui, lakini sikui
nimewahi kusikiasikia kitu kama hicho, hapana, niwe mkweli, sijui kabisa.”
Mkurugenzi wa Shirika la
Wasaidizi wa Kisheria Wilaya ya Kwimba, Mishano Sagalani na Mratibu wa Ukimwi
wilayani humo, Dkt Ally Sadick, wamekiri kuwa PF3 na matumizi yake havifahamiki
kwa wananchi wengi.
“Hata upatikanaji wa PF3
bado ni shida wilayani hapa,” amesema Sagalani huku akitolea mfano kesi za
wasichana watano waliofanyiwa ukatili wa kingongo zilizoripotiwa ofisini kwake
kati ya Mei na Juni mwaka huu akisema kati ya hao, wawili ndio walipata fomu
hiyo kwa ajili ya matibabu na ushahidi mahakamani.
Kwa upande wake, Dkt
Sadick amesema huduma ya PF3 wilayani Kwimba inakabiliwa na changamoto lukuki
zinazohitaji utatuzi ili kuwezesha wahanga wa vitendo vya ukatili kuwa na
ushahidi wa kutosha kutetea haki zao mahakamani.
“Kwenye suala la PF3 kuna
changamoto nyingi, kwanza sio vituo vyote vina wataalamu wa kuijaza, wengi
wanaijaza wanavyoweza, hivyo inakuwa haina ubora unaotakiwa.
“Changamoto nyingine iko
kwenye vituo vya afya, anayepaswa kuijaza ni daktari aliyemwona mhanga siku ya
kwanza,” amesema Dkt Sadick.
Tafsiri ya maneno hayo ya
Dkt Sadick ni kwamba mhanga asipomkuta daktari hukosa huduma ya kujaziwa PF3 na
zinazojazwa kwa uelewa binafsi mtu zinakuwa na upungufu wa vigezo muhimu
vinavyokubalika kwa ushahidi mahakamani.
Katika kutatua tatizo la
uelewa mdogo wa kujaza PF3, daktari huyo ameshauri vyuo husika kuwa na somo
maalumu la ujazaji wa fomu hiyo. “Ni vizuri kwenye vyuo vyetu kuwepo na topic
(kipengele) maalumu ya kujaza PF3,” amesema.
Dkt Sadick amesema kuwa
kwa kufanya hivyo, watapatikana wataalamu wa kujaza PF3 kikamilifu na kwa
usahihi, hivyo kuwezesha wahanga kupata msaada unaostahiki kwa upande wa fomu
hiyo.
Lakini pia, kukosekana kwa
kituo maalumu (One Stop Centre) cha huduma za polisi, matibabu na ustawi wa
jamii kwa wahanga wa ukatili, kunatajwa kuwa ni miongoni mwa vikwazo vya
kukabiliana na vitendo hivyo wilayani Kwimba.
“Huduma hizi zinapokuwa
maeneo tofauti wakati mwingine huwakatisha tamaa wahanga kwa kuona watapata
usumbufu na kuingia gharama kubwa kuzitafuta," amefafanua.
Hata hivyo, Dkt Sadick na
wadau wengine wameshukuru kupata mafunzo ya kupambana na ukatili ukiwamo wa
kingono kwa watoto yanayowezeshwa na Mradi
wa Boresha unaotekelezwa chini ya Ushirikiano wa Kiimani Tanzania (The Tanzania Interfaith Partnership Association
- TIP).
Ushirikiano huo
unaundwa na taasisi nne za kidini ambazo ni Baraza la Wakristo Tanzania (CCT),
Baraza la Kitaifa la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Baraza la Maaskofu Wakatoliki
Tanzania (TEC) na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar (MoZ).
Mchungaji Mathias Mleka wa
AICT Ngudu, Kwimba amesema mafunzo hayo yanawasaidia kuelimisha wananchi
madhara ya vitendo vya ukatili ukiwamo wa kingono kwa watoto katika jamii.
“Tumegundua kwamba watoto
wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kingono katika sherehe na michezo ya ngoma…
tunashukuru mafunzo tuliyopewa na TIP tunaendelea kuyasambaza na mwitikio wa
jamii ni mkubwa,” amesema Mchungaji Mleka.
Mchungaji Mathias Mleka wa AICT Ngudu, Kwimba akizungumza na mwandishi wa Mara Online News (hayupo pichani) mjini Ngudu, hivi karibuni |
Akyoo amesema ukatili wa
kingono kwa watoto unachangiwa na uelewa duni wa wananchi kuhusu madhara ya
vitendo hivyo, mila na desturi zisizozingatia usalama wa mtoto hali ambayo pia
huchangia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika jamii.
Maono ya TIP ni
kutengeneza mtandao thabiti wa kiimani unaochangia uwepo wa jamii ya Kitanzania
yenye afya na kizazi kisicho na Ukimwii.
Maafisa wa Mradi wa Boresha unaotekelezwa chini ya TIP wakifanya mahojiano na waandishi wa habari mjini Ngudu, Kwimba hivi karibuni. |
Kumekuwepo na juhudi
mbalimbali za kupiga vita vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto nchini
Tanzania zikiwamo zinazofanywa na Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili kwa
Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).
Mpango huo wa miaka
mitano, ulianza kutekelezwa mwaka 2017/18 na utafikia kikomo mwaka 2021/22
chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Kwa mujibu wa mchumi
kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Happiness Mugyabuso, mpango huo unalenga
kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2021 ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini
uwe umepungua kwa asilimia 50.
No comments:
Post a Comment