NEWS

Thursday 30 July 2020

Mamlaka zilivyoshtukia mpango wa kumuoza mwanafunzi



KAMA sio mamlaka za serikali na wasaidizi wa kisheria, mwanafunzi Sikujua Masunga (sio jina lake halisi) ambaye ni mkazi wa wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, angekuwa ameolewa, yaani angekuwa mke wa mtu kwa sasa.

Sikujua mwenye umri wa miaka 17, alichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu (2020) katika Shule ya Sekondari ya Mwagi wilayani Kwimba. Hata hivyo, mpaka sasa (Julai 2020) hajaripoti shuleni kutokana na kile kinachodaiwa kuwa kuna mkakati wa kutaka kumuoza.

Inaelezwa kwamba Sikujua amechumbiwa na mwanaume mkazi mkazi wa mkoani Geita na kinachofanyika sasa ni maandalizi ya kumtorosha kutoka Kwimba.

Baada ya kupata taarifa hizo, Mara Online News imefuatilia sintofahamu inayojaribu kumnyima Sikujua haki yake ya kupata elimu. Mtoto huyo anaishi na mzazi mmoja ambayeni mama yake.

Mara online News imefanikiwa kufika nyumbani kwao Sikujua, ingawa hata hivyo, haikumkuta mwanafunzi huyo wala mzazi wake, isipokuwa dada yake aliyejitambulisha kwa jina la Edna, ambaye amekiri kwamba mdogo wake huyo hajaripoti shuleni kwa ajili ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza.

“Sijui kwanini hataki kwenda shule, nilimuuliza akasema hataki shule, mama alipotaka kumnunulia uniform [sare za shule] alikataa akasema hataweza masomo na kwamba mzazi akimlazimisha kusoma atapoteza hela bure,” amesema dada huyo wa Sikujua.

Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinaeleza kuwa Shene ambaye ni mama mzazi wa Sikujua, anashirikiana na familia ya mwanaume anayetaka kumuoa mwanafunzi huyo kumkatisha tamaa ya kusoma.

Njama hizo ziligunduliwa na watetezi wa kisheria wilayani Kwimba, ambao waliliarifu Jeshi la Polisi likaenda kuweka shinikizo kwa mzazi wa Sikujua kuhakikisha kuwa mwanafunzi huyo anaripoti shuleni haraka iwezekanavyo ili kuanza masomo ya kidato cha kwanza.

“Huyo binti mzazi na ndugu zake walimbana asiende shule ili wamuoze kisirisiri, lakini baada ya kuripoti taarifa hizo polisi walikwenda wakamuonya mama yake, lakini cha kushangaza mpaka mwezi huu wa Julai mtoto huyo hajaripoti shuleni,” amesema Mkurugenzi wa Wasaidizi wa Kisheria Wilaya ya Kwimba, Mishano Sagalani katika mazungumzo na Mara Online News wilayani Kwimba, juzi.
Mkurugenzi wa Wasaidizi wa Kisheria Wilaya ya Kwimba, Mishano Sagalani akizungumza na mwandishi wa Mara Online News (hayuko pichani) wilayani humo, juzi.

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Luzela, Musa Malole, ameelezea kushangazwa kwake na taswira ya msichana huyo kutokwenda shule licha ya kumhimiza na mama yake mara kadhaa kuhusu suala hilo.

“Binti huyu yupo tu nyumbani, sijafahamu kama ameolewa, nimekuwa nikimhimiza aende shule lakini haendi,” amesema Malole na kuongeza kuwa anaendelea kushirikiana na mamlaka za serikali kuhakikisha kuwa mtoto huyo anaendelea na masomo yake.

Kwa mujibu wa Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mradi wa Boresha (Boresha Projecti) Wilaya ya Kwimba, Respectson Akyoo, mazingira hayo yanayomzunguka Sikujua yanaweza kuwa ukatili wa kingono unaotishia kumnyima msichana huyo haki yake ya msingi ya kupata elimu, lakini pia unaoweza kumfanya ashindwe kufikia ndoto yake.

Akyoo amesema ukatili wa kingono kwa watoto unachangiwa na uelewa duni wa wananchi kuhusu madhara ya vitendo hivyo, mila na desturi zisizozingatia usalama wa mtoto hali ambayo pia huchangia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika jamii.

Mradi wa Boresha unatekelezwa chini ya Ushirikiano wa Kiimani Tanzania (The Tanzania Interfaith Partnership Association - TIP). Unaoundwa na taasisi nne za kidini ambazo ni Baraza la Wakristo Tanzania (CCT), Baraza la Kitaifa la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Baraza la Maaskofu Wakatoliki Tanzania (TEC) na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar (MoZ).

Maono ya TIP ni kutengeneza mtandao thabiti wa kiimani unaochangia uwepo wa jamii ya Kitanzania yenye afya na kizazi kisicho na Ukimwii.

Mkurugenzi wa Watetezi wa Kisheria, Malole na Mchungaji Mathias Mleka wa AICT Ngudu, Kwimba wanasema TIP imewapatia mafunzo ambayo yanawasaidia kuelimisha wananchi madhara ya vitendo vya ukatili ukiwamo wa kingono kwa watoto katika jamii.

“Tumegundua kwamba watoto wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kingono katika sherehe na michezo ya ngoma… tunashukuru mafunzo tuliyopewa na TIP tunaendelea kuyasambaza na mwitikio wa jamii ni mkubwa,” amesema Mchungaji Mleka.

Kumekuwepo na juhudi mbalimbali za kupiga vita vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto nchini Tanzania zikiwamo zinazofanywa na Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).

Mpango huo wa miaka mitano, ulianza kutekelezwa mwaka 2017/18 na utafikia kikomo mwaka 2021/22 chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Kwa mujibu wa mchumi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Happiness Mugyabuso, mpango huo unalenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2021 ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini uwe umepungua kwa asilimia 50.

(Imeandikwa na Christopher Gamaina, Kwimba)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages