NEWS

Friday 25 September 2020

Kundo: Chagueni CCM ndicho chenye ilani inayotekelezeka

Mgombea ubunge jimbo la Bariadi kwa tiketi ya CCM, Mhandisi Kundo Andrea Mathew (kulia) akijinadi katika mkutano wa kampeni, jana.

 

MGOMBEA ubunge jimbo la Bariadi kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhandisi Kundo Andrea Mathew, amesema mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuli yametokana na mipango mikakati inayotekelezeka.

Mhandisi Mathew ameyasema hayo jana kwa nyakati tofauti kwenye mikutano yake ya kampeni katika kata za Isanga na Sima ambapo ametoa mifano hai ya baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni elimu ya msingi na sekondari bila malipo, ongezeko la vituo vya afya, zahanati na hospitali zikiwemo za rufaa.


 

“Kipindi cha nyuma wanafunzi ambao walikuwa hawana ada ya shule walirudishwa nyumbani lakini katika awamu ya tano ya Rais Dkt John Pombe Magufuli wanafunzi wanasoma bure… ufaulu umeongezeka, mfano mzuri ni mkoa wetu [Simiyu] ufaulu upo juu, tukiangalia barabara zinapitika sasa hivi kwenda mikoa ya jirani na kwetu [mkoani humo] ni masaa kadhaa umeshafika. Chagua CCM kwa maendeleo na mipango inayotekelezeka.

“Siku ya kupiga kura nipeni kura, nipo tayari kuwatumikia, nipo tayari kuwaletea maendeleo, nipo tayari kuikumbusha serikali yangu sikivu kukamilisha ahadi inazoahidi kipindi hiki cha kampeni, tuchagueni sisi [CCM] kwa Maendeleo,” amesisitiza Mhandisi Methew.

Ameongeza kuwa mambo yaliyofanywa na CCM ni makubwa na yanaonekana kwa macho kuanzia sekta za afya, maji, kilimo, elimu na barabara huku akisisitiza kuwa chama hicho ndicho chenye ilani inayotekelezeka.

Mgombea ubunge jimbo la Bariadi kwa tiketi ya CCM, Mhandisi Kundo Andrea Mathew (katikati) katika hekaheka za mikutano ya kampeni zake jimboni, jana.

 

Mhandisi Mathew amewaomba wananchi kuhakikisha Oktoba 28, 2020 wanachagua wagombea wa CCM) kuanzia nafasi ya uais, wabunge na madiwani kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wamechagua maendeleo.

Katika mikutano yake, Mhandisi Mathew ameahidi kuwa akichaguliwa atakikisha anashirikiana na serikali kutengeneza daraja ili wakazi wa mtaa wa Ngashanda waweze kuvuka mto Bariadi, hivyo kuwapunguzia wananchi adha, hususan kipindi cha mvua za masika.

Wananchi wakimshangilia mgombea ubunge jimbo la Bariadi kwa tiketi ya CCM, Mhandisi Andrea Mathew katika mkutano wa kampeni jimboni humo, jana.


Awali, akiwanadi wagombea wa CCM, Mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Bariadi, Juliana Mahongo, amewaomba wananchi wote bila kujaLi itikadi za vyama vyao vya siasa kuwachagua wagombea wa CCM.

“Msiangalie itikadi zenu, chagueni CCM - chama cha kufanya vitu kwa mipango na maendeleo tunayaona, mfano hapa kwetu Bariadi tulianza na visima virefu vya maji, sasa hivi tupo mbioni kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria, tunatekeleza kila kitu hatua kwa hatua,” amesema Mahongo.

 

(Habari na picha zote na Anita Balingilaki, Bariadi)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages