
Dkt. Kebwe Stephen Kebwe
Na Mwandishi Maalumu, Serengeti
Aliyepata kuwa Mbunge wa Jimbo la Serengeti mkoani Mara, Dkt. Kebwe Stephen Kebwe, amerejea kwa mara nyingine tena kuwania nafasi hiyo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Leo Juni 28, 2025, Dkt. Kebwe anatarajiwa kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea ubunge wa Serengeti, safari hii akitaja vipaumbele vyake vya mwelekeo wa maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo kuwa ni pamoja na ujenzi wa chuo cha VETA na uboreshaji wa miundombinu ya barabara.
Akizungumza na Mara Online News leo muda mfupi uliopita, Dkt. Kebwe amesema akiwa mbunge ataibana serikali ijenge VETA kwa ajili ya kuwapatia vijana wa Serengeti mafunzo ya ufundi stadi yatakayowasaidia kujiajiri na kuajiriwa, na hivyo kupunguza utegemezi kwa ajira za serikalini
Kuhusu barabara muhimu zinazounganisha Serengeti na wilaya jirani, amesema atashirikiana na serikali kuhakikisha zinajengwa kwa kiwango cha lami ili kuwarahisishia wananchi usafiri, kuchochea biashara zao na kukuza sekta ya utalii.
Aidha, katika juhudi za kuinua elimu ya sekondari, Dkt. Kebwe amesema ataelekeza nguvu kubwa katika ujenzi wa shule za kidato cha tano na sita angalau mbili hadi tatu kwa kila tarafa ili kuwapunguzia wanafunzi adha ya kutafuta elimu mbali na nyumbani, lakini pia kuongeza ufaulu katika jimbo hilo.
Dkt. Kebwe ametaja kipaumbele chake kingine kitakuwa kushawishi Serikali Kuu kuleta mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Serengeti ili kuimarisha huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wengi vijijini na mijini.
Pia, amesema atahakikisha Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, zahanati na vituo vya afya vinaboreshwa, vifaa tiba na dawa zinapatikana kwa wakati, pamoja na kuendeleza juhudi za kusambaza umeme vijijini ili kuchochea maendeleo na kuinua hali ya maisha ya wananchi.
Mwanasiasa na mtaalamu huyo wa afya ambaye amekuwa mtumishi wa umma kwa muda mrefu, amesema anaingia katika kinyang'anyiro cha ubunge akiwa na dhamira ya dhati ya kushirikiana na serikali pamoja na wananchi kuletea maendeleo ya kisekta.
“Wana-Serengeti mimi hawajawahi kuniangusha, niliwahi kusimama mara ya kwanza nikashinda, hata mwaka 2020 kati ya wagombea 59 niliongoza - japo jina halikurudi.
“Hivyo, naomba wana-Serengeti waniunge mkono, mimi siyo mgeni, mimi siyo mtu wa maneno, ni vitendo,” amesema Dkt. Kebwe, akisisitiza kuwa akipata ridhaa ya chama chake - CCM na baadaye kuchaguliwa kuwa mbunge, atajielekeza zaidi katika miradi mikubwa ya maendeleo itakayogusa maisha ya kila mwana-Serengeti.
No comments:
Post a Comment