NEWS

Saturday 3 October 2020

Walioshiriki kura za maoni CCM wawapiga jeki Waitara, Kembaki

Mgombea ubunge jimbo la Tarime Vijijini kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara (kushoto) akipokea mchango wa kununua mafuta ya gari kutoka kwa makada wa chama hicho, Peter Bhusene (wa pili kushoto) na Nicodemus Keraryo (wa pili kulia). Kulia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Hamis Mkaruka. Mchango huo ni kwa ajili ya kuimarisha kampeni za Waitara na Michael Kembaki anayegombea ubunge jimbo la Tarime Mjini.


BAADHI ya wanachama wa CCM walioshiriki kwenye kura za maoni za kuomba kuteuliwa kugombea ubunge katika majimbo ya Tarime Vijijini na Tarime Mjini, wametoa mchango wa mafuta ya gari lita 500 ili kusaidia kuimarisha kampeni za wagombea ubunge wa majimbo hayo kupitia chama hicho.

 

Wagombea waliopigwa jeki hiyo na majimbo yao yakiwa kwenye mabano ni Mwita Waitara (Tarime Vijijini) na Michael Kembaki (Tarime Mjini).

 

Waliokabidhi mchango huo kwa Waitara ni makada wa CCM walioshiriki kura za maoni katika jimbo la Tarime Vijijini, Peter Bhusene na Nicodemus Keraryo, kwa niaba ya wenzao wanaoshiriki bega kwa bega kufanikisha ushindi wa CCM katika majimbo hayo.

 

Makabidhiano hayo yamefanyika katika ofisi ya CCM Wilaya ya Tarime, mbele ya Katibu wa Wilaya, Hamis Mkaruka, leo Oktoba 3, 2020.

 

Bhusene amesema lengo la mchango huo ni kusaidia kuimarisha kampeni za wagombea hao na hatimaye kupata ushindi mnono katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

 

“Tunaungana ili kupata ushindi wa Waitara - Tarime Vijijini na Kembaki - Tarime Mjini. Pia mchango huu unapanda mbegu ya uzalendo ndani ya chama chetu cha CCM, lakini pia kung’oa na kuchoma mbegu ya usaliti ndani ya chama,” ameongeza Bhusene.

 

Naye Keraryo amesema wamejipanga kuendelea kuwasaidia Waitara na Kembaki kwa hali na mali ili kuhakikisha wanaibuka washindi katika kinyang’anyiro cha ubunge na kuwezesha wananchi wa majimbo hayo kupata maendeleo ya kweli.

 

“Tunahitaji majimbo haya ya Tarime yafanane na rasilimali zilizopo,” amesema Keraryo.

 

Akizungumza baada ya kupokea mchango huo, Waitara ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi), amewashukuru makada wa CCM walioutoa akisema wameonesho uzalendo na upendo wa hali ya juu ndani ya chama hicho.

 

“Hii ni dalili njema ya ushindi ambao sio wa Waitara na Kembaki pekee bali wa CCM na wana-Tarime kwa ujumla, wananchi wetu watarajie kupata maendeleo makubwa baada ya ushindi wetu,” amesema Waitara.

 

Orodha kamili ya majina ya makada wa CCM walioungana kutoa mchango huo wa mafuta kwa ajili ya kuimarisha kampeni za ubunge katika majimbo ya Tarime Vijijini na Tarime Mjini, itachapishwa na Mara Online News baadaye.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages