
------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, ameaanika mafanikio lukuki ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mafanikio hayo yameonesha ari kubwa ya utekelezaji na ukamilishaji wa miradi muhimu katika sekta za afya, elimu, maji, uvuvi, kilimo, nishati na maboresho ya miundombinu ya barabara ili kuinua ustawi wa wananchi kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza katika mkutano maalum na waandishi wa habari leo Julai 18, 2025 jijini Dodoma, Kanali Mtambi amesema mafanikio ya ujenzi wa hospitali, vituo vya afya, zahanati, miradi ya maji, vyumba vya madarasa, miradi ya kilimo na kuwafikishia wananchi nishati ya umeme yanaonekana bayana.

Kanali Mtambi alitolea mfano ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Kwangwa, Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia kilichopo Butiama, pamoja na upanuzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege Musoma.
Amesema katika kipindi cha miaka minne tangu Rais Samia achukue uongozi mwaka 2021, shilingi zaidi ya trilioni 1.3 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali mkoani Mara hadi kufikia Juni 30, 2025.
Baadhi ya miradi ya kujivunia iliyotekelezwa mkoani Mara inajumuisha ujenzi wa hospitali nane za halmashauri za wilaya, Hospitali ya Rufaa ya Musoma, vituo 14 vya afya na zahanati 70.
Akizungumzia sekta muhimu ya madini, Kanali Mtambi amesema upo uwezekano mkubwa kwa siku za usoni kwa mkoa huo kuzalisha mabilionea wengi wanaotokana na sekta hiyo.
Mkoa wa Mara unajivunia uwepo wa mgodi mkubwa wa dhahabu wa Barrick North Mara wilayani Tarime, ambao unaotoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa vijiji jirani.
Hali kadhalika, hivi karibuni serikali iligawa bure leseni 48 kwa vikundi vya wachimbaji wadogo wa madini zaidi ya 2,700 wa mkoa huo, ikiwa ni utekelezaji wa programu ya Minning Better Tomorrow, ambapo mgodi wa Barrick North Mara umeshirikiana na serikali kufanikisha mradi huo wa kurasimisha wachimbaji wadogo - unaotajwa kuwa wa kwanza duniani.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa mkoa, hadi sasa miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 33.8 za Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) zilizotolewa na mgodi huo imeshatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Aidha, amesema mkoa wa Mara umepiga hatua katika sekta ya ardhi ndani ya kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita - kwa kupunguza migogoro ya ardhi kutoka 964 mwaka 2021 hadi 125 mwaka 2025, kutokana na juhudi za serikali za kuboresha mfumo wa umiliki, upangaji na matumizi bora ya ardhi.
Hatua hiyo, amesema imeleta utulivu mkubwa katika jamii, hasa katika maeneo ya vijijini ambako migogoro ya ardhi ilikuwa ikichochea migogoro ya kijamii na kushusha kasi ya maendeleo.
“Tumeweka nguvu kubwa katika kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kwa wananchi na taasisi. Hii imeongeza uelewa, kupunguza migogoro na kuongeza mapato ya halmashauri kupitia kodi ya ardhi,” amesema Kanali Mtambi.
Amefafanua kuwa zaidi ya hati 60,969 za kimila zimetolewa kwa wananchi, sambamba na hati miliki za ardhi 6,743, hatua inayowasaidia wananchi kuwa na uthibitisho wa umiliki, na pia kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha kwa maendeleo yao binafsi na ya familia.
Kwa mujibu wa Kanali Mtambi, pato la mkoa wa Mara wenye idadi ya watu 2,372,015 kwa mujibu wa Sensa ya 2022, limeongezeka kutoka shilingi trilioni 5.3 mwaka 2020 hadi shilingi trilioni 6.8 mwaka 2023.
Shughuli kubwa za mkoa wa Mara unaopakana na Ziwa Victoria ni kilimo, ufugaji, uchimbaji madini, uvuvi na utalii - ambapo unamiliki eneo kubwa la hifadhi maarufu duniani - Hifadhi ya Taifa Serengeti.
No comments:
Post a Comment