Na Christopher Gamaina
chrisgapressman@gmail.com
----------------------------------------
Umuhimu wa uboreshaji daftari
Uwazi katika uchaguzi
chrisgapressman@gmail.com
----------------------------------------
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, imeipa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jukumu la kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura Tanzania Bara.
Aidha, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, na Sheria ya INEC Na. 2 ya Mwaka 2024, zinaitaka Tume hiyo kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili - kati ya uchaguzi mkuu uliomalizika na kabla ya uteuzi wa wagombea kwa uchaguzi mwingine.
Hivyo, katika kutekeleza matakwa hayo ya kikatiba na kisheria, INEC ilizindua uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura - ambao ulifanyika kitaifa mkoani Kigoma, Julai 20, 2024.
Uboreshaji huo unahusisha kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi, na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Pia, wapiga kura waliopo kwenye daftari hilo na ambao wamehama wanapata fursa ya kuhamisha taarifa zao kutoka kata, au jimbo walipoandikishwa awali.
Vile vile, uboreshaji huo unawapa wapiga kura walioandikishwa fursa ya kurekebisha taarifa zao yakiwemo majina, na kupata kadi mpya za mpiga kura kwa ambao kadi zao zimepotea, au kuharibika.
Kwa upande mwingine, uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utaondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye daftari hilo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa Tanzania na kifo.
Kwa upande wa Zanzibar, uboreshaji wa daftari hilo utamhusu mtu yeyote aliyepo Zanzibar ambaye hana sifa za kuandikishwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar lakini anazo sifa za kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo, mtu huyo ataruhusiwa kupiga kura moja ya kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 10 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, wafuatao hawana sifa za kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura:
Mtu aliye chini ya kiapo cha utii wa nchi tofauti na Tanzania, asiye na akili timamu, mgonjwa wa akili, aliye kizuizini kwa ridhaa ya Rais, aliyetiwa hatiani kwa kosa ambalo adhabu yake ni kifo na anayetumikia kifungo kwa kosa ambalo adhabu yake inazidi miezi sita iliyotolewa na mahakama.
Ikumbukwe kwamba uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura hauhusiani na kubadilika kwa jina la Tume ya Uchaguzi, hivyo wenye kadi za mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015, 2019 na 2020 hawahusiki na uboreshaji huo iwapo kadi zao hazijaharibika, au kupotea.
Hata hivyo, imebainika kwamba wapo wapiga kura ambao mpaka sasa wana kadi za karatasi zilizotolewa kabla ya mwaka 2015, hivyo hao wanatakiwa kwenda kwenye vituo husika kuandikishwa upya kwa kuwa mfumo uliotumika wakati huo ni tofauti na mfumo unaotumika sasa.
Ni muhimu kwa kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na zaidi kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kama ilivyotangazwa na INEC.
Umuhimu wa uboreshaji daftari
Umuhimu wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni pamoja na kuhakikisha kwamba uchaguzi unakuwa wa haki na uwazi. Hivyo, kushiriki katika mchakato huo ni hatua ya msingi katika kudumisha demokrasia na uongozi bora nchini.
Faida za uboreshaji wa taarifa za wapiga kura kwenye daftari hilo, ni pamoja na kuimarisha uwakilishi wa kijamii. Uboreshaji huo unatusaidia kuhakikisha kwamba kila mwananchi mwenye sifa za kupiga kura ameorodheshwa ipasavyo.
Hii inahakikisha kwamba kila kundi la kijamii, na kila eneo lina uwakilishi unaostahili katika uchaguzi wa viongozi. Hivyo, uamuzi wa wananchi utakuwa na uwakilishi wa kweli kwa jamii nzima.
Lakini pia, uboreshaji wa taarifa za wapiga kura unaepusha udanganyifu wa kura, kama vile kupiga kura mara mbili, au kutumia majina ya watu ambao hawako hai.
Mfumo wa kisasa na sahihi wa uboreshaji huo unazuia vitendo vya udanganyifu na unachangia katika kuleta uaminifu kwenye mchakato wa uchaguzi.
Faida nyingine ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni kusaidia kupata idadi halisi ya wapiga kura katika kila eneo. Hii ni muhimu kwa kupanga shughuli za uchaguzi, kutekeleza mipango ya usalama na jinsi ya kutoa huduma bora kwa wapiga kura siku ya uchaguzi.
Uwazi katika uchaguzi
Kila mwananchi anapojitokeza kutoa taarifa sahihi, inasaidia kuongeza uwazi na uaminifu katika uchaguzi. Kupitia mchakato huo, wapiga kura wanaweza kuangalia na kuthibitisha kuwa majina yao yameorodheshwa ipasavyo, hivyo kuondoa wasiwasi kuhusu mapungufu, au makosa katika orodha.
Kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura pia ni sehemu ya haki na wajibu wa kiraia. Ni njia ya kutimiza jukumu letu katika jamii na kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu.
Kwa hiyo, kujitokeza kwetu katika uboreshaji wa daftari hilo ni hatua muhimu. Kila mmoja wetu anapaswa kuonesha uwajibikaji na kujitolea kwa maendeleo ya taifa letu.
Ni muhimu kwa Watanzania wote wenye sifa zilizoainishwa kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi yetu kujitokeza na kutoa ushirikiano katika uboreshaji wa daftari hilo.
Tunasisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kwani itasaidia kuhakikisha kwamba uchaguzi ujao utakuwa wa haki, uwazi na utaratibu mzuri. Kila mmoja wetu ana haki na wajibu wa kuboresha demokrasia yetu kwa kujitolea kutoa taarifa sahihi, kuangalia orodha na kushiriki katika shughuli za uchaguzi.
Tukitimiza wajibu wetu huo, tutakuwa tunajenga taifa lenye nguvu, uongozi bora na litakalokuwa mfano mzuri wa kuigwa katika kudumisha haki na uwazi katika mchakato wa uchaguzi.
Kwa pamoja, tunaweza kuhakikisha kwamba kura zetu zinawakilisha haki, na maamuzi yetu yanakuwa na matokeo chanya katika maisha ya wananchi wetu.
Karibu tushiriki katika jitihada hizi muhimu za maendeleo kwa taifa letu. Kujiandikisha kuwa mpiga kura ni msingi wa uchaguzi bora.
No comments:
Post a Comment