NEWS

Sunday 27 December 2020

Shule iliyonufaika na ‘keki’ ya uhifadhi yafaulisha wanafunzi wote

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bunyunyi, Faudha Saidi akimwonesha Mwandishi wa Mara Online News vyumba vilivyojengwa na wananchi kwa ushirikiano na TANAPA.

SHULE ya Msingi Bunyunyi iliyopo katika kijiji cha Hunyari wilayani Bunda, Mara imefaulisha wanafunzi wote 53 waliofanya Mtihani wa Taifa wa Kuhitimu Darasa la Saba mwaka 2020.

 

Shule hiyo ni miongoni mwa shule zilizonufaika na matunda ya uhifadhi baada ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuipatia msaada wa fedha kuunga mkono juhudi za wananchi katika kujenga vyumba viwili vya madarasa.

 

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inafanya kazi chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Twiga, swala na pundamilia wakifurahia mazingira hai ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Mwaka huu tumefaulisha wanafunzi wote 53 (wasichana 28 na wavulana 25). Tunashukuru Hifadhi ya Serengeti kwa kutusadia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa,” amesema Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bunyunyi, Faudha Saidi, katika mahojiano maalumu na Mara Online News, hivi karibuni.

 

Saidi amesema kwamba kabla ya kupata msaada huo, baadhi ya wanafunzi walilazimika kusomea nje juani, lakini pia kukatisha masomo wakati wa mvua. “Kwa kweli msaada huu ni mkubwa maana sasa wanafunzi wetu wameacha kusomea nje,” amesema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bunyunyi, Faudha Saidi akizungumza na Mwandishi wa Mara Online News (hayupo pichani).

Mwalimu Saidi amesema ujenzi wa vyumba hivyo viwili ulitekelezwa mwaka 2018 kwa ushirikiano wa wananchi na Hifadhi ya Serengeti kupitia idara yake ya ujirani mwema.

Makundi ya nyumbu yakivuka Mto Mara ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Hata hivyo, Mwalimu Saidi amesema shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 800 bado inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa.

 

“Shule yetu ilianza mwaka 2015 na bado inahitaji vyumba 18 vya madarasa, vilivyopo kwa sasa ni vinane. Pia tunaomba TANAPA imalizie vyumba hivyo viwili kwa kuweka vigae, madirisha, madawati na meza ili sasa mradi ukamilike,” amesema.

 

Mwalimu Saidi amefafanua kuwa shule ililazimika kuanza kutumia vyumba hivyo kabla havijakabidhiwa rasmi ili kusaidia wanafunzi waliokuwa wakisomea nje.

 

“Tulikuwa hatuna jinsi na vyumba hivi kweli vimetusadia sana hata kama mradi bado haujakabidhiwa,” ameongeza mwalimu huyo.

 

Wanafunzi wa shule hiyo wanasema maisha ya shule yamebadilika baada ya ujenzi wa vyumba hivyo.

 

“Zamani wengine tulikuwa tunakaa nje na wengine darasani lakini kwa sasa wote tunakaa darasasni,” amesema mwanafunzi Beborah Haramnada wa darasa la tano.

 

Hifadhi ya Serengeti imekuwa ikitekeleza miradi ambayo imeibuliwa na wananchi katika vijiji vilivyopo jirani na hifadhi hiyo, husasan katika sekta za elimu, afya, maji na barabara, lakini pia miradi ya kiuchumi iliyo rafiki kwa mazingira kama vile ufugaji nyuki.

Tembo ni miongoni mwa vivutio vikuu vya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
 

Sh zaidi ya milioni 200 zimetumika kutekeleza miradi ya ujirani mwema katani Hunyari katika miaka ya karibuni.

 

“Mbali na kijiji cha Hunyari, miradi mingine imetekelezwa katika kijiji cha Kihumbu. Mfano ni ujenzi wa zahanati,” amesema Ofisa Mtendaji wa Kata ya Hunyari, Bajumaa Saidi.

 

Ofisa Mtendaji huyo amesema mradi mwigine wa ujirani mwema umehusisha ujenzi wa nyumba za walimu katika Shule ya Sekondari ya Hunyari.

 

“Kwenye nyumba za walimu, TANAPA walichangia milioni 60, nyumba zimekamilka, walimu wanafurahia maisha,” amefafanua.

Chui pia ni miongoni mwa wanyamapori wanaoipamba Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
 

Utekelezaji wa miradi ya ujirani mwema umesadia kuwafanya wananchi wanaoshi vijiji jirani na Hifadhi hiyo kutambua umuhimu wa wanyamapori na kuachana na uwandaji haramu.

 

“Uwindaji umepungua kwa kiwango kikubwa kutokana na hii miradi ya ujirani mwema na elimu ya uhifadhi inayotolewa, lakini elimu inapaswa kuendelea kutolewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi,” amesema.

 

Jambo lingine lililowafurahisha wananchi wa kata ya Hunyari, ni mpango wa matumizi bora wa ardhi ulioandaliwa kwa ufadhili wa Hifadhi ya Serengeti kupitia idara ya ujirani mwema katika vijiji vyote vinne ambavyo ni Hunyari, Kihumbi, Mariwanda na Sarakwa.

Simba wakijipumzisha juu ya mti ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Gibita Joseph ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Maraha kijijini Hunyari, amesema miradi ya ujirani mwema ina faida kwa wananchi na uhifadhi. “Tunafurahi miradi ni mizuri na hata imepunguza uwindaji haramu,” amesema.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyangoto, Weibiro Bopambo, measema “Hata wanafunzi wanafurahia matunda ya uhifadhi, wakati wa mvua walikuwa wakipata shida kusomea nje. Tunaomba TANAPA waendelee kutekeleza miradi ya ujIrani mwema.”

 

(Imeandikwa na Mugini Jacob, Bunda)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages