NEWS

Thursday 18 February 2021

Mwenyekiti, Mkurugenzi Serengeti wakanusha upotevu wa mapato

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Mhandisi Juma Hamsini (kushoto) akionesha nakala ya kumbukumbu ya ukusanyaji mapato ya halmashauri hiyo katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake leo Februari 18, 2021. Kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ayub Mwita Makuruma.

MWENYEKITI na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara wamekanusha taarifa ya upotevu wa mapato ya halmashauri hiyo.

 

Wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Mugumu leo Februari 18, 2021, viongozi hao, Ayub Mwita Makuruma (Mwenyekiti) na Mhandisi Juma Hamsini (Mkurugenzi Mtendaji), wamesema taarifa iliyoandikwa kwenye chombo cha habari cha kidijitali kwamba kuna upotevu wa asilimia 80 ya mapato ya halmashauri hiyo ni ya upotoshaji kwa umma.

 

Taarifa hiyo iliyoandikwa jana Februari 17, 2021, ilinukuu Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo lililoketi wiki iliyopita, likilalamikia upotevu wa asilimia 80 ya mapato na kwamba asilimia 20 ya makusanyo ndiyo huingizwa kwenye akaunti ya halmashauri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Mhandisi Juma Hamsini akionesha mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya mtandao kwenye kompyuta wakati wa mkutano huo.

Akitoa ufafanuzi, Makuruma ambaye ndiye aliongoza kikao hicho cha baraza la madiwani, amesema kilichozungumzwa ni tofauti na kilichoandikwa.

 

“Kuhusu kwamba asilimia 80 ya mapato yamepotea hicho kitu hakikuzungumzwa kikaoni, si kweli, inawezekana madiwani walinukuliwa vibaya, tulichozungumza ni kuhusu kushuka kwa makusanyo ya mapato ya halmashauri yetu,” amesisitiza Mwenyekiti huyo wa halmashauri.

 

Kutokana na kushuka kwa makusanyo ya mapato, Makuruma amesema waliunda kamati ya kufuatilia vyanzo vya mapato ikiwa ni pamoja na kubaini visivyojulikana ili viingizwe kwenye mfumo wa halmashauri hiyo.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji, Mhandisi Hamsini amekanusha taarifa hiyo akisema “Taarifa hiyo si ya kweli, sisi Halmashauri ya Serengeti tunafanya vizuri na tunatumia mapato yetu ya ndani kugharimia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.”

 

Hamsini ametoa mfano ya miradi ya karibuni iliyotekelezwa kutokana na mapato ya ndani kuwa ni ujenzi wa stendi ya mabasi ya mjini Mugumu na Hospitali ya Wilaya ya Serengeti.

 

Ameongeza kuwa mapato ya ndani yamekuwa yakitumika kuimarisha sekta ya elimu ambapo idadi ya shule za msingi imeongezeka kutoka 103 hadi 140 na shule za sekondari za umma kutoka 16 hadi 40.

 

“Katika sekta ya afya, tumejenga nyumba za watumishi za two in one katika maeneo mbalimbali kwa kutumia mapato ya ndani,” amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo.

 

Amesema matumizi mazuri ya mapato ndiyo yameiwezesha Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuendelea kupata hati safi kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kila mwaka.

Mkutano huo ukiendelea.

Pia, Hamsini amesema hata mifumo ya ukusanyaji na utumiaji mapato ya halmashauri hiyo imeimarishwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kudhibiti opotevu wa mapato.

 

“Huwezi kuficha hata senti moja," amesema na kuhoji "Kama tungekuwa tunapoteza asilimia 80 ya mapato si halmashauri ingekuwa imefungwa?"

 

Taarifa kamili ya mafainiko yaliyofikiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kutokana na mapato ya ndani itachapwa kwenye gazeti la Sauti ya Mara wiki ijayo.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages