NEWS

Monday 19 April 2021

Mbunge Ghati, chachu ya maendeleo ya kisekta mkoani Mara

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete akihutubia wananchi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani 2021 katika viwanja vya Nyamwaga wilayani Tarime.

HAKIKA amedhihirisha kuwa wanamke wanaweza. Huyu si mwingine yeyote yule bali ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete.

 

Mbunge huyu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameonekana kuwa chachu ya maendeleo ya kisekta ya mkoa wa Mara kwa kipindi kifupi cha miezi takriban mitano tangu aapishwe na kuanza kutekeleza majukumu yake ya kibunge.

 

Katika kipindi hicho kifupi, Ghati ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu, ameweza kuhamashisha kama si kushiriki kwa vitendo shughuli mbalimbali za maeneleo ya wananchi mkoani Mara.

 

Hadi sasa ndiye mbunge mwanamke mkoani Mara anayeonekana kutumia muda wake mwingi katika kuhamasisha na kuchangia gharama za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya elimu.

Mbunge Ghati (kulia) na Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi wakisalimiana kwa bashasha katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, hivi karibuni.
 

Pia, Mbunge Ghati ameonekana kuwa mwepesi wa kuitikia mialiko kutoka vikundi mbalimbali vikiwemo vya wanawake na kuvipiga jeki ya kuviwezesha kujikwamua kiuchumi.

 

Leo itoshe tu kutaja machache miongoni mwa mambo mengi ya kimaendeleo ambayo Mbunge Ghati ameweza kuyafanya mkoani Mara kwa kipindi kifupi cha miezi mitano.

 

Ameweza kutoa fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni moja kuchangia gharama za ununuzi wa mabati ya kuezeka vyumba vya madarasa ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Rorya.

Mbunge Ghati (kulia mbele) akiungana na wanawake wengine kucheza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani 2021 katika viwanja vya Nyamwaga wilayani Tarime.
 

Vile vile, katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuboresha elimu, Mbunge Ghati ameahidi kutoa mchango wa madawati 50 kwa ajili ya shule mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

 

“Lazima tuhakikishe shule ya sekondari ya wasichana Nyamwaga inajengwa ili watoto wetu wapate elimu bora. Akina mama ni jeshi kubwa, ukimuinua mtoto wa kike umeinua jamii nzima, kwa hiyo lazima wanawake tuungane na tuinuane,” amesema Mbunge huyo katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu yaliyofanyika kiwilaya katika viwanja vya Nyamwaga, Tarime.

Mbunge Ghati (katikati) akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa duka la Airtel mjini Musoma, hivi karibuni.


Katika wilaya ya Musoma, Mbunge huyu wa Viti Maalum ameweza kuungana na wanawake kwa hali na mali katika shughuli mbalimbali.

 

Mfano hivi karibuni, ameweza kuwapatia wanawake wa CCT na WAWATA msaada wa viti 100 na mahema mawili kwa ajili ya kuendeleza mradi wao wa kujiongezea kipato.

 

Kama hiyo haitoshi, amewezesha wanawake wajasiriamali zaidi ya 100 kufungua akaunti za Malkia katika Benki ya CRDB Tawi la Musoma - hatua ambayo itawawezesha kupata mikopo ya mitaji ya kuanzisha na kuendeleza miradi yao.

 

Itakumbukwa pia, wakati wa Sikukuu ya Pasaka mwaka huu, mbunge huyu amewapatia wafungwa na mahabusu katika Gereza la Tarime msaada wa mchele.

Mbunge Ghati (katikati) akiwa amevishwa kitenge alichozawadiwa na Umoja wa Wanawake wa CCT na WAWATA wakati wa maomboi ya kitaifa mjini Musoma, hivi karibuni.
 

Mbunge Ghati hajajikita kwenye miradi ya kijamii na kiuchumi pekee, kwani anashiriki pia katika kuchangia maendeleo ya shughuli za kiroho. Kwa mfano, majuzi tu ametoa mamilioni kadhaa ya fedha kuchangia ujenzi wa Kanisa la SDA Nkende wilayani Tarime.

 

Lakini pia, Mbunge Ghati tumemwona na kumsikia akiuliza maswali na kujenga hoja mbalimbali kwa ujasiri Bungeni - zinazolenga kutatua kero na kuwaletea wananchi wa mkoa wa Mara maendeleo.

 

Miongoni mwa maswali aliyouliza ni yale ya kuitaka Serikali kuwapatia wazee wote vitambulisha vya kuwawezesha kupata matibabu bila malipo, lakini pia kutatua tatizo la ukosefu wa dawa katika hospitali za umma.

Mbunge Ghati akifafanua jambo katika mahojiano maalumu na Mara Online News mjini Tarime, hivi karibuni.
 

Kwa ujumla, Mbunge Ghati ameudhihirishia umma kuwa ni kiongozi mahiri na mchapakazi aliye na utayari wa hali na mali katika kuchangia maendeleo ya wananchi wa mkoa wa Mara bila ubaguzi wowote ule.

 

Wananchi wa mkoa wa Mara wanaridhishwa na falsafa ya uongozi wa mbunge huyu na kumtabiria mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kibunge.

 

“Tunampongeza Mbunge wetu Ghati kwa ushirikiano mkubwa wa kimaendeleo anaouonesha kwa wananchi, amekuwa msaada mkubwa sana hata kwa sisi wanawake, tunamwombea aendelee kuwa nyota ya maendeleo mkoani Mara,” amesema mkazi wa mjini Musoma, Sophia Manyama.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

2 comments:

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages