MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye maafufu kwa jina la Namba Tatu, na Mbunge wa mstaafu wa Jimbo la Rorya, Gregory Mogendi Nyanchini, wamezuru katika ofisi za blogu ya Mara Online News na gazeti la Sauti ya Mara - kwa nyakati tofauti leo Aprili 7, 2021 na kueleza kufurahishwa na ubora wa habari zinazoripotiwa na vyombo hivyo.
“Hongereni sana, mnafanya kazi nzuri hata ya kutangaza maendeleo ya mkoa wa Mara na kufichua maovu katika jamii,” amesema Namba Tatu.
Kwa upande wake, mzee Nyanchini ambaye pia ni mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kuwa ni msomaji mzuri wa gazeti la Sauti ya Mara na kuomba waandishi wa gazeti hilo kuelekeza nguvu pia katika kuripoti habari za kuhamasisha kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa.
Mzee
Nyanchini akipitia nakala ya gazeti la Sauti ya Mara toleo la wiki hii
alipotembelea ofisi hizo leo.
Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Sauti ya Mara na blogu ya Mara Online News, Jacob Mugini amewahakikishia viongozi hao kuwa vyombo hivyo vitaendelea kutoa habari bora zinazohamasisha maendeleo endelevu katika sekta mbalimbali.
“Tunafurahi kuona kuwa gazeti letu la Sauti ya Mara sasa limeendelea kuvutia wasomaji wengi wakiwemo wa vijijini ndani na nje ya mkoa wa Mara,” amesema Mugini.
Kwa upande wake, Mhariri Mkuu wa Blogu ya Mara Online News na Gazeti la Sauti ya Mara, Christopher Gamaina amesema wamejipanga kuendelea kuwapa wasomaji habari zenye upekee na ubora wa aina yake.
“Sisi hatuweki tu kila kitu kwenye gazeti, au blogu, mpaka tujue habari tunayochapisha inaenda kuleta mabadiliko gani katika jamii, au katika uhifadhi wa vyanzo vya maji na mazingira. Tumejikita zaidi katika kuhamsisha maendeleo ya kisekta,” amesema Gamaina.
(Habari na picha zote: Mara Online News)
No comments:
Post a Comment