NEWS

Thursday 22 April 2021

Waziri Mkumbo azuru BRELA, aahidi kuwapa watalaamu nafasi ya kuchapa kazi

Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo akisaini kitabu cha wageni katika ofisi ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) jijini Dar es Salaam.
 

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo amesema atatoa nafasi kwa wataalamu ambao ni watumishi wa taasisi zilizo chini ya wizara yake kufanya kazi bila kuwaingilia.

 

Waziri Mkumbo ametoa msimamo huo Aprili 21, 2021 alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) jijini Dar es Salaam ambapo amezungumza na menejimenti na uongozi wa BRELA.

Waziri Mkumbo (kushoto) akiwasili katika ofisi za BRELA. Katikati ni CEO wa BRELA, Godfrey Nyaisa.


“Nataka muelewe kuwa mimi kama waziri wenu mpya lazima nitawapa nafasi ya kufanya kazi za kitaaluma na kitaalamu, sitawaingilia. Tumewasomesha ninyi na ninyi ndio wataalamu wetu,” Waziri Mkumbo amewambia watendaji wa BRELA.

 

Hata hivyo, Profesa Mkumbo amewataka watendaji wa BRELA kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria - akitolea mfano utatuzi wa migogoro katika kampuni.

 

“Katika utendaji wenu mzingatie sheria na kanuni, msitumie busara. Kama mambo yapo mahakamani acha mahakama imalize na msilete kwa waziri mnatafuta busara,” ametahadharisha.

 

Waziri Mkumbo ameahidi ushirikiano wa kutosha kwa BRELA katika kuiwezesha kufikia malengo yake.

 

“Niwahakikishie ushirikiano wa kutosha na ninyi [BRELA] mtupe (wizara) ushirikiano,” amesisitiza.

Waziri Mkumbo (kushoto) akipokewa katika ofisi za BRELA jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni CEO wa BRELA, Godfrey Nyaisa akitambulisha wafanyakazi wenzake kwa Waziri Mkumbo.

 

Waziri huyo ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wafanyabiashara wa Tanzania kurasimisha biashara zao kwa kuzisajili ili waweze kunufaika zaidi.

 

Amesema kuna ripoti ameisoma ikionesha nchini Tanzania kuna biashara ndogo na za kati milioni 3.7 lakini kati ya hizo ni 147,580 sawa na asilimia nne zimesajiliwa.

 

Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa BRELA, Godfrey Simango Nyaisa amemwambia Waziri Mkumbo kuwa usajili wa kampuni kwa sasa unafanyika kwa saa chache baada ya mfumo husika kuboreshwa.

 

“Zile zama za kutumia wiki au mwezi kusajili kampuni, BRELA tumehama. Kama documents (nyaraka) ziko sahihi siku haiwezi kuisha bila mteja kusajili kampuni yake,” amesema CEO Nyaisa.

CEO Nyaisa akizunguma katika kikao cha Waziri Mkumbo. 

 

Nyaisa ameongeza kuwa baadhi ya wateja wameanza kufurahia mfumo huo kwa kutumia saa chache kufanya usajili wao kwa njia ya mtandao.

 

(Habari: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages