Maparachichi |
KATIKA gazeti lake la kilimo, TAHA inasema “Kilichoko mezani kwako ndiyo afya yako. Taasisi hii inayojishughulisha na kilimo cha mbogamboga na matunda inasisitiza kwamba katika nyakati hizi ambapo dunia inapambana na janga la Covid-19, suala la kujiimarishia kinga ya mwili halina mjadala.
Pengine tukijua hali halisi, tutafanya maamuzi sahihi. Kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Lishe cha Taifa (TFNC) ya mwaka 2018, mkoa wa Mara ulikuwa wa nne (asilimia 35.7) baada ya Mwanza, Simiyu na Geita kwa kuwa na wanawake wenye udhaifu wa afya (anaemic).
Aidha, utafiti huo ambao ulichapishwa June 2019, ulibaini kwamba mkoa wa Mara ni wa nane kati ya mikoa ambayo ina watoto wenye utapia mlo uliokubuhu (severe malnutrition).
Ni ukweli usiopingika kwamba binadamu wote wanastahili mlo unaojitosheleza. Lakini akina mama wanapaswa kupewa kipaumbele katika lishe kwa sababu ndio wenye jukumu la uzazi na malezi na hivi huwafanya kuwa kwenye kundi hatarishi. Inabidi wao wenyewe walitambue hilo na ikibidi wajihudumie.
Watoto nao wasipolishwa vizuri, miili yao pamoja na akili vitadumaa. Huu ni mzigo kwa taifa, na kinga ni bora kuliko tiba.
Hatusemi kwamba ukosefu wa matunda pekee ndio unaoathiri afya ya jamii, bali unachangia kwa kiasi kikubwa tatizo hili.
Kilimo cha matunda kinaweza kubadili taswira hii kwani mkulima akivuna hata kama ni mazao ya biashara, huwa hasau nyumbani.
Iwapo jamii itajikita katika kilimo cha matunda ya muda mfupi kama vile papai (miezi 6), au matikiti maji (miezi 2 hadi 3), tunaweza kuona matokeo chanya.
Mkulima mmoja anadokeza katika blogu yake kwamba kama masharti ya kilimo yakizingatiwa, ekari moja ya matikiti maji inaweza kumwingizia mkulima Shilingi milioni tano.
Anaongeza kwamba hiki ni kilimo endelevu na mkulima anaweza kulima mara tatu hadi nne kwa mwaka.
Mkoa wa Mara una wilaya zenye rutuba nzuri kama vile Tarime, Serengeti, Musoma Vijijini, Rorya, Bunda na Butiama. Pia ina mabonde mazuri na mito, ukiwepo mto maarufu wa Mara.
Akizungumzia kilimo cha matikiti maji, Siproza Charles Nyadhi ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia maji ya mto Mara Kaskazini, inayojumuisha vijiji vinane wilayani Rorya, anasema wakulima walijaribu kulima matikiti maji lakini mvua ziliponyesha kwa wingi, walikata tamaa maana walipata hasara kubwa.
Matikiti maji
Hata hivyo, Kanuni Kanuni ambaye ni Afisa Miradi wa Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) Mkoani wa Mara, anatoa angalizo kwa wakulima.
"Ni lazima wakulima wabadili taratibu zao, wawe na kalenda ya uzalishaji. Kwanza sio lazima wawe na zao moja kwa wakati mmoja ili bidhaa isifurike sokoni. Waelewe nyakati gani za kupanda nini," anasema Kanuni na kubainisha kuwa Shirika la WWF linatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wakulima kujua mbinu mbalimbali za kilimo na masoko katika muktadha wa mnyororo wa thamani.
"Tunawaunganisha na SIDO na mamlaka nyingine kama BRELA na TMDA ili wajue jinsi ya kusajili bidhaa zao," anasema Kanuni.
Pamoja na changamoto mbalimbali, soko la matunda, hasa matikiti maji maparachichi (ovacado) ni pana, lipo wazi wakati wote. Jiji la Dar es Salaam peke yake na viunga vyake ni soko la kutosha kwa mazao hayo.
Kuna viwanda vikubwa vya kusindika matunda kama S.S. Bakhresa na Motsun Group ambao wanahitaji matunda kwa wingi.
Pia kuna fursa ya soko la matunda mbalimbali katika migodi ya madini mkoani Mara ukiwemo ule wa North Mara unaojishughulisha na uchimbaji wa dhahabu wilayani Tarime.
Migodi ni mojawapo ya maeneo yenye fursa za soko la matunda mkoani Mara
Lakini pia kuna soko kubwa la matunda katika hotel za kitalii zilizopo Serengeti mkoani Mara ambazo zinaweza kufikiwa hata kama watatoa maelekezo wangetaka matunda yawe ya kiwango gani.
Kwa mujibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, kuna hoteli na kambi za kitalii zaidi ya 160 katika maeneo ya uhifadhi wilayani humo, zenye uhitaji mkubwa wa matunda kwa ajili ya wageni.
Mojawapo ya hoteli za kitalii zilizopo Serengeti
Ni wakati mwafaka wa kuchangamkia fursa hizi ili kilimo cha matunda kiwe endelevu na chenye tija.
(Imeandikwa na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment