NEWS

Monday 10 May 2021

Masharti ya kimila yasaidia kisima cha maji kudumu miaka 90



Mti ujulikanao kwa jina la Iketontira umechangia uhifadhi wa kisima cha maji cha asili ambacho kimedumu kwa miaka 90 sasa katika kijiji cha Keisangora wilayani Tarime, Mara.

VYANZO vya maji vya asili vikihifadhiwa na kutunzwa vizuri vinaweza kuhudumia jamii kwa miaka mingi bila kukauka, imethibitika.

Hali hiyo imedhihirika katika kisima kinachofahamika kwa jina la Ghonyi kilichopo katika kijiji cha Keisangora wilayani Tarime, Mara ambacho kimedumu kwa miaka 89 bila kukauka maji.

Inaelezwa kwamba siri ya uendelevu wa kisima hicho ni uzingativu wa sheria za kimila za ulinzi na matumizi ya vyanzo vya maji.

“Kisima hiki kiligunduliwa na kuanzishwa mwaka 1932 wakati wa kiangazi kikali kilicholazimu baadhi ya wananchi kwenda kunywesha mifugo yao Migori nchini Kenya,” anasema mzee wa mila wa kijiji cha Keisangora, Chacha Mniko katika mazungumzo na Sauti ya Mara kijijini hapo, wiki iliyopita.

Mniko anafafanua kuwa kisima hicho kilianzishwa chini ya usimamizi wa wazee wa mila ambao waliweka taratibu za ulinzi na matumizi yake.

Anataja baadhi ya masharti yaliyowekwa kuwa ni pamoja na marufuku ya kata miti ya asili inayokizunguka, tumia vyombo vichafu kuchota maji, kuoga na kunywesha mifugo katika kisima hicho.

Mzee huyo anasema watu wote wameendelea kutii taratibu zilizowekwa hali ambayo imekiwezesha kuwa endelevu na msaada mkubwa katika jamii inayokizunguka.

Francis Maseke na John Panga ambao nao ni wazee wa mila katika kijiji cha Keisangora, wanasema Ghonyi ni miongoni mwa visima 20 vya maji vya asili vilivyoteuliwa kuhudumia wananchi wa koo ya Wairegi inayoishi Mashariki mwa wilaya ya Tarime.

Kwa mujibu wa Mjumbe wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) na Mhazini wa Jumuia ya Watumia Maji ukanda wa Tigite Juu, Penina Chacha, kisima hicho kwa sasa kinahudumia maelfu kadhaa ya wakazi wa kijiji cha Keisangora na vijiji jirani bila tozo ya fedha.


Kutoka kulia ni wazee wa mila, Francis Maseke, Chacha Mniko, John Panga na Mjumbe wa LVBWB, Penina Chacha wakizungumza na wanahabari katika eneo la kisima cha Ghonyi.

Wakazi wa kijiji hicho, Ester Bhoke na Neema Mwita wanakiri kuwa kisima hicho hakijawahi kukauka maji hata misimu ya kiangazi ambayo mamia ya wananchi kutoka vijiji jirani huongezeka kwa ajili ya kuchota maji.

Mara Online News imefika kilipo kisima hicho na kushuhudia kikiwa kimezungushiwa uzio wa nyaya jirani na mti mkubwa wa asili uitwaa Iketontira kwa lugha ya Kikuria ambao ni miongoni mwa miti rafiki ya vyanzo vya maji.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Keisangora, Simeon Magacha anasema ofisi yake inashirikiana na wazee wa mila kueneza elimu ya uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji vya asili kikiwemo kisima hicho cha Ghonyi.

“Elimu hii inahusisha uondoaji wa miti isio rafiki kwa vyanzo vya maji na tuna kamati ya ulinzi na usalama wa vyanzo vya maji kijijini hapa,” anasema Magacha na kubainisha kuwa wamepata elimu hiyo kutoka kwa wadau wa uhifadhi endelevu wa vyanzo vya maji ikiwemo LVBWB.

Wazee wa mila, Maseke, Mniko na Panga wanasema mkakati wa kuondoa miti isiyo rafiki kwenye vyanzo vya maji umepata mwitikio mkubwa wa wananchi na wengi wameanza kuutekeleza kijijini Keisangora.

Mmoja wa wanakijiji walioanza kutekeleza mkakati huo kwa vitendo ni Matiko Rogena ambaye amekata miti yote inayozuiwa jirani na vyanzo vya maji katika shamba lake mseto linalopakana na eneo la kisima hicho.

“Kama unavyoona mwenyewe katika shamba langu hili nimeshakata miti yote tuliyoambiwa siyo rafiki kwenye vyanzo vya maji, nimebakiza ambayo haina madhara,” Rogena anaieleza Mara Online News.


Mzee Rogena akionesha sehemu ya eneo aliloondoa miti isiyo rafiki kwa chanzo cha maji katika shamba lake kijijini Keisangora.

Afisa Uhusiano wa LVBWB, Mhandisi Gerald Itimbula anapongeza jitihada zinazofanywa na wakazi wa kijiji cha Keisangora katika kuhifadhi na kutunza vyanzo vya maji na kuahidi kuendelea kuwawezesha katika kuimarisha uendelevu wa vyanzo hivyo.

“Tutaendelea kuwapatia wananchi wa kijiji hiki elimu na hata vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kutekeleza mikakati ya kuimarisha utunzaji wa vyanzo vya maji ukiwemo huu wa kuondoa miti isiyo rafiki kwenye vyanzo vya maji,” anasema Mhandisi Itimbula.


Mhandisi Itimbula akielezea umuhimu wa wadau kushirikiana katika ulinzi na utunzaji wa vyanzo vya maji vya asili, alipozungumza na waandishi wa habari jirani na kisima cha Ghonyi.

Pamoja na mahitaji mengine, wazee wa mila katika kijiji hicho wanaomba mamlaka husika zikiwemo LVBWB na Serikali kuwapatia vitambulisho maalumu vitakavyowahalalisha na kuongezea nguvu katika usimamizi wa mikakati ya ulinzi na utunzaji wa vyanzo vya maji.

(Habari na picha: Christopher Gamaina wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages