NEWS

Sunday 16 May 2021

Mto Mara unavyotegemewa kwa kitoweo cha samaki na changamoto za wavuvi



Mvuvi akionesha samaki aina ya kamongo mara baada ya kumvua katika mto Mara, leo Mei 16, 2021 asubuhi.

LICHA ya kuwezesha upatikanaji wa kitoweo na mapato kwa mamia ya wananchi wa kawaida wanaoishi jirani na mto Mara upande wa Tanzania, sekta ya uvuvi inakabiliwa na changamoto mbili kubwa; ambazo ni ukosefu wa zana za kisasa za uvuvi wa samaki na ongezeko la magugu maji katika mto huo.

Wakazi wa kijiji cha Kwisaro kilichopo wilaya ya Butiama mkoani Mara ni miongoni mwa wananchi ambao wameendelea kufurahia kitoweo cha samaki wanaovuliwa kutoka mto Mara.

Tatu Stephen ni mmoja wa wakazi wa kijiji cha Kwisaro ambaye anasema hawajawahi kukosa kitoewo cha samaki wanaovuliwa katika mto Mara.

“Sisi hapa [Kwisaro] samaki sio shida na wanatoka mto Mara hapa jirani,” Tatu ameambia Mara Online News kijijini Kwisaro, wiki iliyopita.

Ametaja samaki kama moja ya faida kubwa ambayo yeye na wananchi wingine wa Kwisaro wanaipata kutokana na uwepo wa mto Mara.

“Faida ya mto Mara kwetu ni samaki, na mbali na kitoweo ni chanzo cha mapato kwa wanawake na vijana,” Tatu ambaye ni mama wa watoto kadhaa amesema.

Wananchi wa kijiji cha Kwisaro wanasema kuna aina mbalimbali ya samaki wanaopatikana mto Mara kama vile kambare (mumi), kamongo, nembe na sato.

“Kuna aina nyingi za samaki katika mto Mara ambao hata hatuwafahamu, lakini samaki ni wengi na wanapatikana kwa bei nafuu,” amesema Thomas Marwa ambaye pia ni mkazi wa kijiji cha Kwisaro.


Kijana akionesha samaki aina ya kambare (mumi) waliovuliwa katika mto Mara

Marwa anasema samakii mmmoja anauzwa kijijini hapo kuanzia Shilingi 500 na kuendelea kutegemeana na ukubwa wake. “Ukipata samaki wa Shilingi elfu tano huwa mkubwa - anatosha familia kula na kubaki,” anesema.

Hivyo Mara Online News imebaini kuwa moja ya kitoweo kikubwa katika kijiji cha Kwisaro na vijiji jirani ni samaki wanaopatikana mto Mara.

Kazi ya kuvua samaki katika vijiji hivyo inafanywa na vijana wa kiume na wanawake hufanya kazi ya kununua samaki hao kwa vijana na kuwauza sokoni.


Wanawake wa kijijini Kwisaro wakiuza samaki wa aina mbalimbali wanaovuliwa katika mto Mara

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Mara Kusini, Mairi Magabe, Kwisaro ni moja ya vijiji viliovyo chini ya jumuiya hiyo ambavyo bado vinafurahia matunda ya mto Mara kutokana na uwepo wa samaki.

“Ingawa samaki wamepungua lakini bado hali ya upatikanaji wa samaki katika kijiji cha Kwisaro ni nzuri na vijiji vingine kama vile Wegero, Kirumi, Kongoto na Ryamisanga inaridhisha,” anasema Magabe ambaye Jumuiya yake ina majukumbu ya kusimamia matumizi endelevu ya vyanzo vya maji ukiwemo mto Mara.

Hata hivyo, wavuvi katika vijiji hivyo wanakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na zana za kisasa za uvuvi wa samaki.

“Yaani wanatumia zana duni na hata mitumbiwi ambayo pia ni duni na wakati mwingine inaweka maisha ya wavuvi hatarini,” anaeleza Mairi.

Changamoto nyingine ni uwepo wa magugu maji ambayo yanawanyima wavuvi uhuru wa kuvua samaki katika mto huo ambao hutiririsha maji ndani ya Ziwa Victoria upande wa Tanzania.

“Magugu maji ni kikwazo kikuba sana, tunaomba mamlaka husika kuangalia tatizo la magugi maji ili wavuvi wasiendelee kupata shida wanapokuwa kazini,” amesema Mairi.

Mkurugenzi wa Shirika la Wakulima na Wavuvi (VIFAFIO) Kanda ya Ziwa, Majura Maingu anasema ufumbuzi wa changamoto ya magugu maji kwa wavuvi hao upo mikononoi mwao.

“Kinachotakiwa kwa hawa wavuvi ni kuunda vikundi vya kung’oa na kuchoma magugu maji, hili limefanyika Ziwa Victoria na kuonesha mafanikio,” Majura ameiambia Mara Online News.

Kuhusu tatizo la zaana duni za uvuvi, ameshauri wavuvi hao kutumia zana zinazokubalika kama vile ndoana baadala ya kokoro.

“Pengine wanatumia kokoro ndio maana wanapata shida wakati wa kuvua kwenye maeneo yenye magugu maji,” ameongeza Maingu.

Afisa Uvuvi katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Shesheku Kivaria anasema wananchi hao wanahitaji mitumbwi ya kisasa na elimu ili waweze kufanya uvuvi endelevu.

“Elimu inahitajika juu ya matumizi ya ndoano katika maeneo yale na sio nyavu, lakini pia mitumbwi wanayotumia sio salama,” Kivaria ameiambia Mara Online News.

Amesema pia kuna umuhimu wa kutoa elimu ya kufuga samaki badala ya kutegemea uvuvi ndani ya mto pekee yake.

“Tungepata wadau, wananchi wangesaidiwa kuanzisha ufugaji wa samaki kuliko kutegemea mto na hapo wangeongeza kipato,” amesema Afisa Uvuvi huyo.

Bonde la mto Mara lina mchango mkubwa katika ustawi wa maisha ya watu zaidi ya milioni 1.1 katika nchi za Tanzania na Kenya.


Sehemu ya mto Mara katika wilaya za Butiama na Rorya

Hivi karibuni, Tanzania imezindua mpango wa ugawanaji maji katika bonde la mto Mara ikiwa ni hatua itakayosadia kulinda viumbe hai ndani ya mto huo na kuendeleza sekta muhimu za kiuchumi.

Mpango huo pia utasaidia kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji kwa kukomesha migogoro kuhusu matumizi ya maji na kukabiliana na tishio la kimazingira linalotokana na ongezeko la idadi ya watu na shughuli za binadamu katika bonde hilo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba amezindua mpango huo jijini Mwanza, Aprili 24, 2021 kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga.

Katika hotuba yake, Mhandisi Kemikimba amewapongeza wadau wote waliofanikisha uandaaji wa mpango huo akisema utasaidia kusimamia matumizi endelevu ya maji na yenye tija katika bonde la mto Mara.

“Mto huu ni muhimu sana kwa ikolojia katika bonde la Mto Mara na huchangia maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii pamoja na uhifadhi wa uoto wa asili,” amesema Naibu Katibu Mkuu huyo na kuagiza utekelezaji wa mpango huo uanze haraka na uwe na mrejesho chanya. “Tupate detailed action plan (utekelezaji wa kina wa mpango kazi),” amesisitiza.

 

Wavuvi wa samaki katika mto Mara wanatarajia kwamba watafikiwa na mpango wa Serikali wa kuhamasisha uvuvi wa kisasa na endelevu katika mito na maziwa ya asili kama ilivyoanishwa kwenye tovuti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi (www.mifugouvuvi.go.tz).

Eneo la bonde la mto Mara lina ukubwa wa kilomita za mraba 13,325 huku mto wenyewe ukiwa na urefu wa kilomita 400.

Mto huo ambao ni shirikishi kwa nchi za Tanzania na Kenya huanzia milima ya Mau na kupita katika Hifadhi ya Maasai Mara upande wa Kenya, kisha kupita Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Tanzania) na kumwaga maji yake katika Ziwa Victoria upande wa Tanzania.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages