NEWS

Sunday 16 May 2021

Serikali kuanzisha maabara ya upimaji wa sampuli za madini mkoani MaraWaziri wa Madini Tanzania, Doto Biteko akifungua mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini mkoani Mara kuhusu namna bora ya kuchukua sampuli za uchunguzi na uchenjuaji wa madini, mjini Musoma, leo.

SERIKALI imetangaza mpango wa kuanzisha maabara ya upimaji wa sampuli za madini mkoani Mara ili kusogeza huduma hiyo karibu na wachimbaji wadogo wa madini mkoani humo.

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyasema hayo wakati akifungua warsha ya siku tatu kwa wachimbaji wadogo wa madini mkoani Mara, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na kufanyika kwenye ukumbi wa uwekezaji mjini Musoma, leo Mei 16, 2021.

Waziri Biteko amesema maabara hiyo itaongeza ufanisi katika upimaji wa sampuli za madini katika mkoa wa Mara ambao ameutaja kuwa una mchango mkubwa kwa pato la Taifa linalotokana na uzalishaji madini.

Ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha mazingira ya wachimbaji wadogo mkoani Mara baada ya kukamilisha ujenzi wa masoko matatu ya dhahabu mkoani humo.


Sehemu ya wachimbaji wadogo wa madini wakiwa kwenye ukumbi wa mafunzo mjini Musoma

Waziri huyo ametumia nafasi hiyo pia kukemea vitendo vya utapeli wa madini na majungu miongoni mwa wachimbaji wadogo wa madini mkoani Mara na kuwataka kupendana na kushirikiana katika juhudi za kutumia sekta hiyo kujijenga kiuchumi.

Ameishukuru GST kwa kuandaa mafunzo hayo akisema yatawaongezea wachimbaji hao uelewa masuala ya madini na ufanisi katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Hata hivyo, Waziri Biteko amewataka watendaji wa taasisi hiyo kuelekeza nguvu kubwa katika kuwatembelea na kuwaelimisha wachimbaji wadogo kwenye maeneo ya migodi yao badala ya kukaa ofisini.


Waziri Biteko (wa kwanza kushoto waliokaa), Afisa Madini wa Mkoa wa Mara, Nyaisara Mgaya (wa kwanza kulia waliokaa) na baadhi ya wachimbaji wadogo waliohudhuria mafunzo hayo.

Awali, Mjiolojia Mwandamizi kutoka GST na Mratibu wa Mafunzo kwa Wachimbaji Wadogo Taifa, John Kalimenze amemweleza Waziri Biteko kwamba mafunzo hayo yatawajengea wachimbaji hao uelewa juu ya namna bora ya uchukuaji wa sampuli za uchunguzi na uchenjuaji wa madini.

Akizungumza na Mara Online News nje ya ukumbi wa mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Wanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mara, Boniface Ndengo amesema sekta ya madini ina fursa kubwa ya uwekezaji na hivyo ametoa wito kwa wananchi wenye mitaji ya biashara kujitokeza kuzichangamkia.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages