NEWS

Monday 31 May 2021

Zifahamu Hifadhi za Taifa Kanda ya Magharibi na raha ya kuzitembelea



Watalii wakifurahia kutazama na kupiga picha makundi ya nyumbu katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti

WANANCHI wameomba kuungana na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika ulinzi na uendelezaji wa Hifadhi za Taifa zilizopo Kanda ya Magharibi kwa ajili ya utalii na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Wito huo umetolewa na Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi wa TANAPA Kanda ya Magharibi, Martin Loibooki katika mahojiano maalum na Mara Online News ofisini kwake mjini Bunda mkoani Mara, hivi karibuni.

Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi wa TANAPA Kanda ya Magharibi, Martin Loibooki

Loibooki amesema utalii ni zao la uhifadhi endelevu wa wanyamapori na mazingira, huku akitaja faida za kutembelea Hifadhi za Taifa kuwa ni pamoja na kujionea vivutio mbalimbali, kujifunza masuala ya wanyamapori na mazingira hai, kupiga picha za kumbukumbu na kuchangia uhifadhi endelevu kwa maendeleo ya Taifa.

Ametaja Hifadhi za Taifa zilizopo Kanda ya Magharibi kuwa ni Serengeti, Gombe, Kigosi, Milima ya Mahale, Burigi-Chato, Ibanda Kyerwa, Rumanyika Karagwe, Kisiwa cha Rubondo, Kisiwa cha Saanane na Mto Gala.


Chui ndani ya Serengeti

Kwa mujibu wa Loibooki, ushirikiano wa wananchi na TANAPA katika ulinzi wa hifadhi hizo utawezesha wanyamapori kuongezeka na kuchochea utalii wa picha.


Twiga ni miongoni mwa wanyamapori wanaopamba Hifadhi za Taifa Kanda ya Magharibi

“Ninaomba wananchi waunge mkono juhudi za Serikali katika uhifadhi endelevu… hifadhi hizi ni fursa ya maendeleo na utalii,” amesema Loibooki na kuongeza:

“Watanzania tuko wengi, hivyo tukitembelea hifadhi zetu tutakuwa na mchango mkubwa kwa ajili ya uhifadhi endelevu wa hifadhi zetu za Taifa.”

Kamishna Mwandamizi huyo wa uhifadhi amesema TANAPA Kanda ya Magharibi itaendelea kuhamasisha Watanzania kutembelea Hifadhi za Taifa zilizopo ndani ya ukanda huo. “Bahati nzuri kuna hifadhi mama na bora Afrika ambayo ni Serengeti,” amesema.


Simba wa Serengeti

Mbali na kupata tuzo ya hifadhi bora Afrika, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imeingizwa kwenye orodha ya Maajabu Saba ya Dunia. Mojawapo ya vivutio vikuu katika hifadhi hii ni misururu ya nyumbu wanaovuka Mto Mara kwenda Mbuga ya Maasai-Mara na kurudi Serengeti kila mwaka.

Ukitembelea Hifadhi za Taifa Kanda ya Magharibi utajionea vivutio mbalimbali na kusuuza moyo, utajifunza masuala ya wanyamapori na mimea, utapiga picha za kumbukumbu na utachangia uhifadhi endelevu kwa maendeleo ya Taifa.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages