NEWS

Monday 31 May 2021

Waziri Mkuu: Mkoa wa Mara una maji ya kutosha kwa ajili ya viwanda, kilimo
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Muongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Mara

MKOA wa Mara una maji ya kutosha kuwezesha maendeleo ya viwanda na kilimo chenye tija kwa wananchi na Taifa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema.

Majaliwa amesema hayo katika hotoba yake ya uzinduzi wa Muongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Mara mjini Musoma, Mei 28, 2021.

“Maji yapo ya kutosha Mara, hivyo uwekezaji kwetu ni rahisi, kama unahaitaji maji yapo kwa ajili ya viwanda na kilimo,” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Vyanzo vya maji mkoani Mara ni pamoja na Ziwa Victoria na Mto Mara ambao pia ni sehemu muhimu ya uendelevu wa ikolojia ya Serengeti.

Sehemu ya Mto Mara katika mpaka unaotenganisha wilaya za Rorya na Butiama

Waziri Mkuu Majaliwa amesema mkoa wa Mara pia umejaaliwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba inayostawisha mazao ya aina mbalimbali kama vile kahawa, miwa, chai, mkonge na ndizi, hivyo ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa hizo.


Waziri Mkuu Majaliwa (wa pili kutoka kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Muongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Mara. Wa kwanza kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Robert Gabrien na wa tatu kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye “Namba Tatu”

Ofisi ya Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) imekuwa ikitoa elimu na kuhamasisha uhifadhi endelevu wa Bonde la Ziwa Victoria na Mto Mara kwa ustawi wa maisha ya wananchi na ikolojia ya Serengeti ambayo ni kivutio kikuu cha utalii nchini.

LVBWB imekuwa ikifanya hivyo kwa vitendo na kupitia kaulimbiu yake inayosema “Ziwa Letu, Uchumi Wetu, Tulitunze”.


Ziwa Victoria ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya maji mkoani Mara

Mto Mara unaanzia nchini Kenya na unatirisha maji ndani ya Ziwa Victoria upande wa Tanzania.

Hivi karibuni, wakazi wa vijiji vilivyopo kandokando ya Mto Mara katika wilaya ya Butiama mkoani Mara, wameishukuru Serikali kupitia LVBWB kwa kuwezesha kutunza vyanzo vya maji ukiwemo mto huo.

LVBWB imenunua miche ya miti zaidi 30,000 kutoka jumuiya ya watumia maji ya Mara Kusini kwa Shilingi milioni tisa.

“Tayari miche hiyo imepandwa katika vijiji vilivyo kandokando ya mto Mara na tunaishukuru Serikali kwa kununua miche hiyo kwetu,” Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Mairi Magabe ameiambia Mara Online News, hivi karibuni.


Upandaji miti ni muhimu kwa hifadhi ya vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla

Magabe ameongezea “Mbali na kandokando ya mto Mara, miche mingine imepelekwa kupandwa katika wilaya jirani za Serengeti na Bunda.”

Mara Kusuni imekuwa jumuiya ya kwanza kuzalisha miche katika bonde la mto Mara upande wa Tanzania. Baadhi vijiji vilivyo chini ya jumuiya hiyo ni Kwisaro, Kirumi na Kitasakwa.

Magabe amesema lengo lao ni kuufanya mradi wa kuzalisha miche kuwa endelevu kama watapa soko la kuiza.


Uoteshaji miche ya miti kwenye vitalu ni miongoni mwa miradi inayoendelea kupewa msukumo mkubwa mkoani Mara
 

Magabe ameongeza kuwa jumuiya hiyo pia inaendelea kupata ushirikiano mzuri kutoka LVBWB, jambo ambalo linawatia moyo wananchi wa vijiji hivyo kuendelea kutunza bonde la Mto Mara na mazingira kwa ujumla.

“Tumepewa elimu ya kutunza vyanzo vya maji na Bodi ya Maji [LVBWB] imetupatia usafiri wa uhakika wa pikipiki,” amesema Magabe ambaye ni miongoni mwa wananchi wa wilaya ya Butiama ambao suala la utunzaji wa Bonde la Mto Mara ni kipaumbele chao.

LVBWB imetoa usafiri wa pikipiki za kisasa kwa jumuiya kadhaa za watumia maji ili kuongeza ufanisi katika utunzaji na usimamizi wa rasilimali za maji katika ngazi za vijiji, hatua ambayo imeonesha mafanikio makubwa.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages