NEWS

Monday 10 May 2021

Ujerumani yaipa Tanzania bilioni 56 kupunguza makali ya Covid-19 sekta ya utalii



Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Regina Hess (kulia), Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Damas Ndumbaro (kushoto mbele), Katibu MKuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt Allan Kijazi (katikati mbele), Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Kanda ya Magharibi, Martin Loiboki (kushoto nyuma) na viongozi wengine wakati wa ziara katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

SERIKALI ya Ujerumani imetangaza kuipatia Tanzania Euro milioni 20 (sawa na Shilingi bilioni 56) ikiwa ni msaada wa dharura (emergency funding) wa kusaidia kupunguza makali ya Covid-19 katika sekta ya utalii.

Mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuendeleza shughuli za uhifadhi.

Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Regina Hess ametangaza kutolewa kwa msaada huo mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, juzi (Jumamosi) Mei 8, 2021.

Hess amesema fedha hizo zitatumika kugharimia uhifadhi wa ikolojia katika Hifadhi za Taifa za Serengeti na Nyerere, lakini pia Pori la Akiba la Selous.

Nyumbu ni miongoni mwa vivutio vikuu vya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Amefafanua kuwa msaada huo ambao umepewa jina la Emergency Funding for Conservation of Biodiversity Support, umebuniwa kutokana na madhara ya mlipuko wa virusi vya corona katika sekta ya utalii.

Janga la corona duniani limepunguza idadi ya watalii na hivyo kusababisha mapato yatokanayo na utalii katika maeneo yaliyohifadhiwa kama Serengeti kupungua kwa kiasi kikubwa.


Balozi Hess (kulia) na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Damas Ndumbaro wakiwa eneo la kituo cha wageni ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Sekta ya utalii imeathirika sana na tunahitaji kweli kusadia, na fedha hii itaenda Serengeti, Nyerere na Seleous,” Balozi huyo wa Ujerumani amewambia waandishi wa habari.

Amesema msaada huo wa utaliwezesha Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuendelea na kazi za uhifadhi.


Kutoka kushoto ni Waziri Ndumbaro, Balozi Hess na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa TANAPA, Pascal Shelutete (kulia) katika ziara hiyo.

Katika ziara hiyo, Balozi Hess na Waziri Ndumbaro wamefuatana pia na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Kanda ya Magharibi, Martin Loiboki, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Masana Mwishawa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa TANAPA, Pascal Shelutete.

Kutoka kulia ni Balozi Hess, Waziri Ndumbaro na Ofisa Uhusiano wa Ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Dkt Katrin Bomemann ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Pia wadau wengine kutoka FZS na Kfw (Benki ya Maendeleo ya Ujerumani) wameshiriki katika ziara hiyo ambayo imempa Balozi Hess na Waziri Ndumbaro fursa ya kutembelea miradi ya uhifadhi ambayo imekuwa ikifadhiliwa na Serikali ya Ujerumani ukiwemo mradi wa kutokomeza nyaya za kutega wanyamapori wakiwemo nyumbu.

Balozi Hess na Waziri Ndumbaro wametumia fursa hiyo pia kukagua mazingira ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kutumia ndege ndogo na kutembelea Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya IKONA ambako wamepata taarifa kuhusu uendeshaji wa Jumuiya hiyo ambayo pia inatajwa kukabiliwa na ukata mkubwa kutokana na madhara ya janga la Covid -19 katika sekta ya utalii.


Waziri Ndumbaro (katikati) akielekeza jambo katika ofisi za Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya IKONA. Wa pili kulia ni Balozi Hess.

 


Meneja Mradi wa FZS Tanzania, Masegeri Rurai (kulia) akiwaonesha Waziri Ndumbaro na Balozi Hess ramani ya IKONA WMA.



Balozi Hess (kulia) akifurahia baada ya kukabidhiwa zawadi na katika ofisi za FZS ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakati wa ziara hiyo.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages