NEWS

Monday 10 May 2021

Bonanza la kuhamasisha utalii wa kushuhudia matukio makubwa ya nyumbu katika Hifadhi ya Serengeti lafana BundaMkuu wa Wilaya ya Bunda, Mwalimu Lidia Bupilipili (mwenye suruali nyekundu) akizungumza na wanamichezo kwenye uwanja wa Sabasaba mjini Bunda lilipofanyika bonanza la kuhamasisha utalii wa ndani katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

HIFADHI ya Taifa ya Serengeti imeshirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali na Serengeti Safari Marathon kufanikisha bonanza la kuhamasisha wananchi kwenda kufanya utalii wa ndani, hususan kushuhudia matukio makubwa ya nyumbu kuelekea mwishoni mwa mwezi huu wa Mei, 2021.

Bonanza hilo limefanyika jana Mei 9, 2021 katika viwanja vya Sabasaba mjini Bunda ambapo limehusisha burudani na mashindano ya michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, ngoma za asili na kufukuza kuku.


Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mwalimu Lidia Bupilipili (mwenye kofia nyeupe), wadau wa na wachezaji wa timu za Bunda SC na Bajaj FC katika picha ya pamoja kwenye uwanja wa Sabasaba mjini Bunda.

Kwa mujibu wa Afisa Mhifadhi Mkuu na Mkuu wa Kitendo cha Utalii wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tutindiga George, matukio yatakayoshuhudiwa ni ya nyumbu kupandanda kwa ajili ya mimba na kuvuka katika eneo la Magharibi mwa hifadhi hiyo.

“Matukio hayo yatafanyika Mei 22 na 30, mwezi huu [Mei], hivyo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti tunawakaribisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia vivutio hivi kwa gharama nafuu,” amesema Mhifadhi Tutindiga.


Mhifadhi Tutindiga George

Mhifadhi huyo amefafanua kuwa utaratibu uliowekwa unamtaka mwananchi kulipa Sh 39,500 kwa ajili ya kugharimia nauli ya kwenda na kurudi, kiingilio na chakula cha mchana ndani ya Hifadhi.

Akihutubia wakati wa bonanza hilo la kuhamasisha utalii wa ndani, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mwalimu Lidia Bupilipili amesema idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza katika tukio hilo ni ishara ya utayari wao wa kwenda kushuhudia matukio hayo ya nyumbu na vivutio vingine katika hifadhi hiyo.


Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mwalimu Lidia Bupilipili (kulia) akihutubia wananchi katika bonanza hilo.


Mkuu wa Wilaya, Mwalimu Bupilipili (kushoto) na wadau wa utalii wakifurahia jambo wakati wa bonanza hilo.

“Mimi nitakuwa wa kwanza, natoa wito kwa wananchi wenzangu kujitokeza kwa wingi twende kutalii na kusuuza nyoyo zetu kwa kujionea vivutio vya utalii katika hifadhi yetu ya Serengeti,” amesema Bupilipili.

(Habari na picha zote: Christopher Gamaina wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages