NEWS

Monday 31 May 2021

Wavuvi Mto Mara wawezeshwe kufanya uvuvi wa kisasa, wenye tija



Mmoja wa wavuvi katika Mto Mara akiwa akionesha samaki aina ya kambale (mumi) aliowavua kama alivyokutwa na camera ya Mara Online News kando ya mto huo eneo la daraja la Kirumi, hivi karibuni.

MOJAWAPO ya maliasili zinazochangia ustawi wa jamii mkoani Mara ni Mto Mara, ambao pamoja na kuinua shughuli za kilimo, pia ni chanzo cha samaki ambao ni bidhaa adhimu kwa chakula na biashara.

Mto Mara huanzia kwenye milima ya Mau nchini Kenya na husafiri kilometa 400 kabla ya kuingia Ziwa Victoria upande wa Tanzania.

Mto huu hububujisha maji yake katika wilaya za Serengeti, Tarime, Butiama na Rorya nchini Tanzania na kutengeneza Bonde la Mto Mara lenye kilomita za mraba 13,325 na wakazi wasiopungua 1,100,000.

Pamoja na ukweli kwamba mto huu una samaki wengi, bado wavuvi wengi wanaoishi kwenye kingo zake, hawajaweza kufaidika ipasavyo kutokana na rasilimali hii.

Kilio chao kikubwa ni magugu maji ambayo yamevamia Mto Mara kwa kasi. Kana kwamba hiyo haitoshi, wavuvi pia wanalalamikia zana duni kama vile mitumbwi, wakisema ni vigumu kupata samaki wengi kwa jinsi hali ilivyo.

Wavuvi wengine, ambao wanajumuisha kina mama pia, wanatamani kupata mafunzo ya uvuvi wa kisasa ili waboreshe hali ya maisha yao.

"Samaki ni wengi mtoni na bei ni nzuri. Hata ukiwa na shilingi 500 tu, unapata samaki wa kukutosha," anasema Tatu Stephen, mkazi wa kijiji cha Kwizaro wilayani Butiama na kuongeza kuwa kinachokwamisha wavuvi ni magugu maji na teknolojia duni ya shughuli za uvuvi.

"Ukitumia ndoano utapata kiasi kidogo cha samaki, sana sana kwa siku moja hata beseni halijai. Hatuna utaalamu wa kisasa," anasema Tatu.

Akizungumzia adha hiyo, mkazi mwingine wa eneo hilo, Thomas Marwa naye anasema kero kubwa ni magugu maji yanayoenea kwa kasi. Lakini pia zana duni na ukosefu wa mbinu za kisasa vimechangia kurudisha nyuma shughuli za uvuvi.

"Siku hizi hata kina mama wanavua samaki. Lakini hawana zana za kisasa kama vile mitumbwi ya uvuvi. Magugu maji nayo ni hatarishi kwani mitumbwi haiwezi tena kuelea majini," anasema Thomas.

Aina ya samaki wanaovuliwa Mto Mara ni wengi lakini wanaojulikana zaidi ni kambale, sato na kamongo.

Naye Mairi Magese ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Mara Kusini, anasema tatizo la magugu maji linadumaza shughuli za uvuvi na anaonya kwamba wavuvi hawana uwezo wa kupambana na uoto huo unaoenea kwa kasi.

Wavuvi wana zana duni. Hawawezi kuondoa magugu maji," anasema Mairi.

Lakini Mkurugenzi wa Shirika la Wavuvi Kanda ya Ziwa, Majura Maingu anaonekana kuleta suluhisho la magugu maji kwa kuwataka wavuvi waanzishe vikundi ili waweze kung'oa magugu maji.

"Wavuvi wanaweza kuondokana na changamoto hii kwa kuanzisha vikundi vya kupambana na magugu maji kama walivyofanya katika Ziwa Victoria," anasema Majura.

Ni jambo la kutia moyo kuona kwamba Serikali imeonesha dhamira ya kuweka msukumo katika shughuli za uvuvi kwa kupanga kuanzisha mabwawa ya kuzalisha vifaranga bora wa samaki aina ya sato na kambale, kuhamasisha jamii iunde vikundi vya ufugaji samaki na kutoa elimu ya uhifadhi mazingira na viumbe wa majini.

Lakini ingekuwa vema kama dhamira hii nzuri ingeambatana na kutafuta ufumbuzi wa kero ya magugu maji katika Mto Mara.

Kama wavuvi wa eneo hili wana zana duni na elimu finyu ya uvuvi na ufugaji samaki wa kisasa, ni wazi kwamba uwezo wao wa kupambana na magugu maji ni duni pia. Wasipopata hamasa ya kuendeleza shughuli hii muhimu, inawezekana wakaiacha na kutafuta mbinu nyingine za kujikimu kimaisha.

Ikumbukwe kwamba Mto Mara ni hazina kubwa kwa wakazi wa mkoa wa Mara. Ni mto unaosafiri kilometa nyingi kuwaletea riziki ya chakula na biashara.

Samaki ni bidhaa adimu na ghali kwa mikoa mingi Tanzania, licha ya kwamba ina faida lukuki za lishe ya jamii. Ina protini nyingi zinazopokewa kirahisi na mwili wa binadamu.

Samaki pia ana mafuta yenye kiambata Omega3 kinachomfanya binadamu kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, kutunza kumbukumbu na kuishi muda mrefu, kwa mujibu wa wataalamu wa lishe.

Hivyo, sauti hizi za wakazi wa maeneo yanayopitiwa na Mto Mara hazina budi kufanyiwa kazi, ili kufanya shughuli za uvuvi wa samaki kuwa endelevu na zenye tija kwa wananchi hao.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages