NEWS

Saturday 29 May 2021

TRA Mara yateketeza bidhaa za 311m/-Bidhaa bandia zikiteketezwa kwenye jalala la Manispaa ya Musoma kwa usimamizi wa TRA Mkoa wa Mara, wiki hii.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara imeteketeza kwa moto bidhaa bandia zenye thamani ya Sh milioni 311 zilizokuwa zinaingizwa nchini kwa magendo kupitia mpaka wa Sirari wilayani Tarime.

Akiongoza kikosi kazi katika tukio hilo kwenye jalala la Manispaa ya Halmashauri ya Musoma wiki hii, Kaimu Meneja Msaidizi wa TRA Mkoani hapa, Nuhu Msangi alisema bidhaa hizo zilikamatwa na kikosi kazi cha kuzuia magendo mpakani hapo.

“Hizi bidhaa bandia zikiwemo sigara ambazo hazijulikani mtengenezaji wake wala tarehe ya kuharibika, mafuta ya kula, bangi na tumbaku tunaziteketeza kwa sababu hazina viwango vya ubora kwa matumizi ya binadamu,” alisema Msangi.

Mkaguzi wa usalama wa chakula kutoka ofisi ya Mkemia wa Mkoa, Fadhili Shedani alitoa wito kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanaagiza bidhaa halali ili kuepuka kuingia hasara kwa kama hiyo.

“Bidhaa hizi kama zingetumika kwa watu zingeleta madhara kwa afya, ni vizuri wafanyabiashara kuuza bidhaa zinazokidhi usalama na wapitishe njia halali ili zikaguliwe,” alisema Shedani.

Akizungumzia bidhaa hizo, Mkaguzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kituo cha Sirari, Pascal Peter aliwataka wafanyabiashara kuwa wazalendo kwa nchi yao.

“Nawashauri wafanyabiashara wazingatie sheria na wapitishe njia sahihi, hapa tuna bidhaa ambazo zimeisha muda wake kama mahindi na sigara ambazo hazioneshi zimetoka wapi wala kiwango cha sumu kilichopo,” alisema Peter.

Kaimu Afisa Afya wa Manispaa ya Musoma, Magreath Kazaura alitoa wito kwa jamii kuhakikisha wanakagua na kujiridhisha na ubora wa bidhaa na inakotoka kabla ya kununua.

“Siyo vizuri binadamu kutumia bidhaa ambazo hazijulikani usalama wake kwani zinaweza kuleta kansa mwilini, ni wito wangu kwa jamii kabla hujanunua kitu kikague,” alisisitiza Kazaura.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages